Kwa nini nchi za Afrika zinaongoza katika orodha ya mataifa karimu zaidi duniani?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kulingana na utafiti wa Charities Aid Foundation (CAF) World Giving Report 2025, uliofanywa kwa kuwashirikisha zaidi ya watu 50,000 kutoka nchi 101, walifanyautafiti kuhusu mapato ya watu na uwiano wa ufadhili wanaotoa kwa mashirika ya misaada na watu wenye uhitaji.

Nchi sita kati ya kumi zinazoongoza kwa ukarimu zaidi duniani ziko Afrika bara ambalo watu wake hutoa wastani wa 1.6% ya mapato yao, ikilinganishwa na 0.6% pekee barani Ulaya.

Mataifa haya yanaenda kinyume na fikra kuwa ukarimu unatokana na utajiri baliunachangiwa na roho ya kutoa.

Hii hapa ni orodha ya nchi 10 zenye ukarimu mkubwa zaidi duniani.

1. Nigeria : 2.83 %

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Nchini Nigeria, 89% ya watu walitoa fedha mwaka 2024, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi cha ukarimu miongoni mwa mataifa 101 zilizofanyiwa utafiti, huku ikishikilia nafasi ya kwanza duniani katika viashiria vingi vya ukarimu.

Wakazi wa nchi hiyo hutenga wastani wa saa 13.5 kwa mwaka, kwa shughuli za kujitolea, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ya wastani wa dunia wa takribani saa tisa.

Ripoti hiyo inaangazia nafasi muhimu ya desturi za kidini, kama vile zaka, sadaka za kanisani, na michango ya kidini, ambazo zimejikita kwa kiasi kikubwa katika maisha ya kila siku.

2. Misri: 2.45%

Misri inashikilia nafasi ya pili duniani, kutokana na kiwango cha juu cha imani ambacho wananchi wake waziwekea taasisi za misaada ya kijamii, ambazo zinaonekana kuwa miongoni mwa taasisi zinazoaminika zaidi nchini humo

3. Ghana : 2.19 %

Ghana inashikilia nafasi ya tatu duniani pamoja na China.

Nchi hii imejumuishwa miongoni mwa mataifa yenye ukarimu mkubwa kutokana na kiwango cha mapato ambayo wananchi wake hutenga kwa ajili ya kusaidia wengine, pamoja na utamaduni wake wa kushirikiana na kusaidiana katika jamii.

Kama ilivyo katika maeneo mengine ya bara Afrika, misaada ya moja kwa moja kwa watu wenye mahitaji na michango ya kidini ndiyo inayotawala zaidi katika utamaduni wa ukarimu nchini Ghana, kuliko michango inayotolewa kwa taasisi au mashirika yasiyo ya kiserikali.

3. China: 2.19%

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kama nchi pekee isiyo ya Afrika iliyoshika nafasi ya juu katika orodha hii (isipokuwa nchi za Ghuba), China inaonyesha kwamba ukarimu wa mtu au taifa si lazima uambatane na kipato chake.

Ripoti hiyo inaashiria kuwa mataifa yenye kipato cha juu hutoa misaada ya wastani ukilinganisha na kipato chao.

5. Kenya : 2.13 %

Kenya inaonekana kuwa na utamaduni mkubwa wa mshikamano wa kijamii na kusaidiana katika jamii. 86% ya wananchi walitoa fedha kwa sababu mbalimbali za kijamii.

Pia inafaa kuzingatiwa kwamba karibu nusu ya Wakenya wamewahi kushiriki katika shughuli za kujitolea.

6. Uganda: 2.04%

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kama ilivyo nchini Kenya na Tanzania, utamaduni wa kutoa umejikita katika mshikamano wa kijamii, huku idadi kubwa ya watu wakiripoti kuwa na hisia kubwa ya kuwa sehemu ya jamii yao.

7. Falme za Kiarabu: 1.92%

Falme za Kiarabu ni miongoni mwa nchi chache zenye kipato cha juu ambazo hutoa misaada kwa kiwango kinacholingana na nchi zenye kipato cha chini. Ripoti hiyo inaeleza kuwa hatua zinazochukuliwa na serikali zina nafasi kubwa katika hali hii.

Takriban watu 9 kati ya 10 wanaamini kuwa serikali ina ushawishi chanya katika sekta ya misaada ya kijamii, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ya wastani wa dunia wa 36%.

7. Qatar: 1.92%

Kama ilivyo katika Falme za Kiarabu, raia wa Qatar wana Imani na mashirika ya kijamii nchini humo, jambo ambalo limeonekana mara kwa mara kuwa sababu muhimu miongoni mwa nchi za Ghuba zinazoshika nafasi za juu katika orodha hii.

India: 1.92%

.

Chanzo cha picha, Getty Images

India ndiyo nchi pekee kubwa kutoka Asia Kusini iliyoingia katika orodha ya nchi 10 zinazoongoza kwa ukarimu duniani.

Hii inathibitisha kwa ujumla utendaji mzuri wa bara la Asia, ambako wastani wa kiwango cha utoaji wa misaada 1.28% unazidi kwa kiasi kikubwa wastani wa utoaji wa dunia wa 1.04%.

10. Malawi : 1.80 %

Malawi inafunga orodha ya nchi 10 zinazoongoza kwa ukarimu zaidi duniani, na tena inathibitisha mtindo wa ukarimu unaoonekana katika bara la Afrika.

Licha ya kuwa na moja ya viwango vya chini zaidi vya mapato ya kitaifa miongoni mwa nchi zilizoorodheshwa, Malawi hutenga sehemu kubwa zaidi ya mapato yake kwa ajili ya misaada ya kijamii kuliko nchi nyingi zenye utajiri mkubwa zaidi barani Ulaya na Asia Mashariki.

Kwa nini Afrika inaongoza katika orodha hii?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ripoti hiyo inabainisha mambo kadhaa yanayofanana ambayo yanaeleza kwa nini nchi za Afrika zimefanya vizuri katika orodha hii:

Mshikamano wa kijamii na uhusiano wa jamii

Katika nchi ambazo zaidi ya 80% ya wananchi wanasema wanahisi kuwa sehemu kubwa ya jamii yao katika eneo husika, wastani wa utoaji wa misaada hufikia 1.7% ya mapato. Kundi hili linaundwa hasa na nchi za Afrika na Asia.

Imani kwa mashirika ya kijamii

Takribani 75% ya Waafrika wanaamini kuwa mashirika ya kijamii yana mchango muhimu katika jamii zao, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kuliko eneo lolote jingine duniani.

Mtazamo kuhusu nafasi ya serikali

51% ya Waafrika wanaamini kuwa serikali zao zinahamasisha utoaji wa misaada, ikilinganishwa na wastani wa dunia wa 40%.

Utoaji wa moja kwa moja na wa kidini badala ya kupitia taasisi

Barani Afrika, utoaji wa misaada mara nyingi hufanyika kupitia msaada wa moja kwa moja kwa watu wenye mahitaji na kupitia njia za kidini. Aina hizi mbili za ukarimu zilikuwa mara nyingi hazionekani kikamilifu katika tafiti za zamani zilizolenga zaidi michango kwa mashirika yasiyo ya kiserikali

Uhusiano kati ya utajiri na ukarimu

Kwa kiwango cha dunia, nchi zenye kipato cha chini hutenga wastani wa 1.45% ya mapato yao kwa ajili ya misaada ya kijamii, ikilinganishwa na 0.70% katika nchi zenye kipato cha juu.

Afrika inaonyesha wazi hali hii, ambapo licha ya kuwa na rasilimali za kifedha zilizo finyu, nchi nyingi za bara hili zinaonyesha viwango vya juu vya ukarimu na mshikamano wa kijamii.