Moja kwa moja, Iran yasema haitakubali kutishwa na Marekani, lakini iko tayari kwa mazungumzo

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema kuwa Iran haitawahi “kupiga magoti” baada ya karibu miezi saba ya vita dhidi ya Marekani na Israel, huku akisisitiza kuwa Tehran iko tayari kufikia suluhisho la kidiplomasia la mzozo huo.

Muhtasari

Iran yasema haitakubali kutishwa na Marekani, lakini iko tayari kwa mazungumzo

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. BASATA yawachukulia hatua Harmonize, Nandy na waandaaji wa mashindano ya urembo

    Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemtaka msanii Rajab Abdul Kahali, maarufu kama Harmonize, kuchukua hatua za kurekebisha ukiukwaji wa maadili baada ya kutuhumiwa kusambaza video ya wimbo wake “Kudos”, ambayo kwa mujibu wa Baraza hilo inakiuka maadili ya Mtanzania na heshima ya wasikilizaji na watazamaji.

    Kwa mujibu wa BASATA, Harmonize hakuwasilisha utetezi wala maelezo ya ziada kabla ya uamuzi kutolewa. Baraza hilo limemuamuru kuiondoa video hiyo kwenye mitandao yake ya kijamii, kulipa faini ya shilingi milioni tano ndani ya siku 14 na kusitisha shughuli za sanaa hadi atakapotekeleza masharti hayo.

    BASATA pia imemchukulia hatua mkurugenzi wa video hiyo, Kennedy David Sanga, baada ya kubaini kuwa alikiuka maadili ya sanaa kwa kuiongoza video hiyo. Ameamriwa kuiondoa video hiyo, kulipa faini ya shilingi milioni tano ndani ya siku 14 na kusitisha shughuli za sanaa hadi atakapotekeleza masharti hayo.

    Wakati huo huo, msanii Faustina Charles Mfinanga, maarufu kama Nandy, amepigwa faini shilingi milioni tatu za Tanzania baada ya kukiri kosa la kuvaa mavazi yasiyo na staha alipokuwa akitumbuiza katika fainali ya Miss Universe Tanzania 2026.

    BASATA imesema Nandy tayari ameiondoa video hiyo na kulipa faini hiyo, hivyo ameruhusiwa kuendelea na shughuli zake za sanaa chini ya uangalizi wa Baraza hilo.

    BASATA pia imewatoza faini waandaaji wa mashindano mawili ya urembo.

    Avil Contractors Company Ltd, waandaaji wa Miss Grand Tanzania, wametozwa faini ya shilingi milioni tatu kwa kuendesha shindano hilo bila kibali cha tukio kutoka BASATA.

    Kwa upande wa Millen Privé & Co. Lifestyle Limited, waandaaji wa Miss Universe Tanzania, wametozwa faini ya shilingi milioni tatu za Tanzania na kupewa onyo kali.

  2. Wanajeshi 8 wa Marekani walijaribu kujiua ndani ya meli ya kivita ya USS Abraham

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kaimu Katibu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, Hong Kao, amefichua kuwa wanajeshi wanane waliokuwa kwenye meli ya kubeba ndege ya USS Abraham Lincoln walijaribu kujiua wakati wa safari ya muda mrefu ya kikazi.

    Kauli hiyo ilitolewa Jumanne kupitia barua aliyomwandikia Seneta Kirsten Gillibrand wa New York, ambaye alikuwa ameibua maswali kuhusu hali na ustawi wa wanajeshi waliokuwa kwenye meli hiyo.

    Familia za wanajeshi hao tayari zilikuwa zimeeleza wasiwasi kuhusu afya ya akili ya wanamaji, ambao walikuwa wakikabiliwa na misheni ndefu, mazingira magumu na msongo wa mawazo. Meli ya Abraham Lincoln ilikuwa imepelekwa katika misheni tangu Novemba mwaka jana na ilikuwa Mashariki ya Kati katika operesheni za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran. Kwa sasa, meli hiyo iko njiani kurejea Marekani.

    Katika barua hiyo, Kao alisema kulikuwa na makasisi watano wa kijeshi pamoja na wataalamu kadhaa wa afya ya akili waliokuwa ndani ya meli hiyo ili kushughulikia mahitaji ya kiroho na kisaikolojia ya wanajeshi. Kwa mujibu wake, watu hao wanane waliojaribu kujiua hawakuwa tu wafanyakazi wa Abraham Lincoln, bali pia walitoka katika kikosi cha anga, kikundi cha mashambulizi, waharibifu wa majini na vitengo vingine vya usaidizi.

    Ingawa Jeshi la Wanamaji la Marekani limewahi kukiri kuwepo kwa changamoto za kiutendaji, limepuuza dhana kwamba kulikuwa na mzozo mkubwa wa afya ya akili ndani ya meli hiyo iliyokuwa na takribani wanajeshi 5,000.

    Kao pia alisema taarifa kuhusu mifumo ya mabomba iliyoharibika na uhaba mkubwa wa chakula kipya zilitiwa chumvi. Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa hitilafu za mabomba katika baadhi ya maeneo, matatizo katika mitambo ya kuondoa chumvi kwenye maji ya bahari na upungufu wa chaguo la vyakula kwa kipindi fulani.

    Kwa upande wake, Seneta Gillibrand aliikosoa serikali ya Trump kwa namna ilivyoshughulikia malalamiko hayo hapo awali, akisema kuwa kuwahudumia wanajeshi kwa namna hiyo ni “jambo lisilokubalika kabisa.” Kwa mujibu wake, matatizo yaliyokuwa yakitajwa kuwa ni “habari za uongo” kwa kweli yalikuwa hali nzito iliyokuwa ikiendelea kuwa mbaya kwa wanajeshi.

    Abraham Lincoln iliondoka California Novemba mwaka jana. Misheni yake ilipangwa kumalizika mwezi Mei, lakini ikaongezwa mara kadhaa. Mwezi Agosti, USS George Washington ilitumwa Mashariki ya Kati kuchukua nafasi ya Abraham Lincoln, ambayo ilikuwa imemaliza misheni ya miezi tisa.

    Kwa mujibu wa takwimu, kujitoa uhai ni miongoni mwa sababu kuu za vifo katika Jeshi la Wanamaji na Jeshi la Wanamaji la Marekani. Utafiti uliochapishwa Januari 2025 na kuwahusisha wanajeshi 956 wa majini ulibaini kuwa wanajeshi wanaohudumu kwenye meli wako katika hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na msongo mkali wa kisaikolojia ikilinganishwa na wanajeshi wa matawi mengine ya jeshi la Marekani.

    Utafiti huo unaonyesha kuwa mazingira duni ya kuishi, kelele za mara kwa mara, ratiba ngumu za kazi na ukosefu wa muda wa kutosha wa kupumzika na kulala ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuathiri vibaya afya ya akili.

    Soma zaidi:

  3. Iran yatoa onyo kali kwa majirani wanaotekeleza vikwazo vya kufunga anga zao

    d

    Chanzo cha picha, IRIB

    Mohsen Rezaei, katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, amezionya nchi jirani na Iran katika mahojiano na televisheni ya Iran kwamba “iwapo zitaungana na vikwazo vya Marekani dhidi ya safari za anga, viwanja vyao vya ndege pia havitaweza kuendesha safari za ndege.”

    “Hamuwezi kuzuia safari za wafanyabiashara wetu, ndege zetu zishindwe kufanya safari na bidhaa zetu zishindwe kuingia kupitia anga, halafu ninyi mkashirikiana na Marekani na sisi tuangalie tu?” alisema.

    Vikwazo vya Marekani dhidi ya mashirika ya ndege ya Iran vimeanza kutekelezwa leo. Safari nyingi za ndege za Iran kwenda nchi mbalimbali zimesitishwa, ingawa baadhi ya nchi bado zinaruhusu mashirika ya ndege ya Iran kutumia viwanja vyao vya ndege.

    Mohsen Rezaei pia amesema taarifa kuhusu mazungumzo na ujumbe mbalimbali pembezoni mwa mkutano wa Umoja wa Mataifa “si mazungumzo, bali ni uwasilishaji tu wa masharti.”

    Amesema hakuna masharti mapya yaliyoongezwa wala yaliyopunguzwa, na kwamba Mlango-Bahari wa Hormuz hautafunguliwa hadi masharti hayo yatakapoondolewa.

    Rezaei amesisitiza kuwa Iran “imewasilisha masharti saba, si matatu.”

    Amesema maafisa wa Iran walikubaliana kuhusu hilo kwa siku mbili au tatu, na wakaafikiana kuwa watawaeleza wapatanishi masharti ya Iran.

    Soma pia:

  4. Tigray yakana kuanzisha mashambulizi, hofu ya kurejea kwa vita yazuka

    d

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Ubalozi wa Marekani nchini Ethiopia umeituhumu TPLF kwa kuanzisha mashambulizi makubwa ya kijeshi. Katika taarifa iliyotolewa, Septemba 23, 2026, Balozi wa Marekani nchini Ethiopia, Ervin J. Massinga, alisema amesikitishwa kuona uongozi wa TPLF, ambao Marekani iliwekea vikwazo mapema mwaka huu, ukifanya “uamuzi usio sahihi wa kuanzisha mashambulizi makubwa.”

    Hata hivyo, uongozi wa eneo la Tigray umekanusha vikali tuhuma hizo. Makamu wa rais wa eneo hilo, Amanuel Assefa, alielezea kauli ya balozi huyo katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii kuwa “ya kukatisha tamaa sana,” huku akiishutumu Marekani na wajumbe wa Umoja wa Afrika kwa kupuuza athari za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani pamoja na mashambulizi ya mara kwa mara ya anga yanayofanywa na kile alichokiita “utawala wa kidikteta.”

    Amesema mashambulizi ya mabomu yamesababisha “vifo vingi vya raia” huko Tigray, akieleza hali ngumu wanayokabili mamia ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao na wanaoishi katika kambi za muda.

    “Ni vigumu kuelewa jinsi kuhamishia lawama upande mwingine kwa namna hii kunavyoweza kuchukuliwa kuwa ni haki,” Amanuel aliandika, akiongeza kuwa wasiwasi kuhusu kutokuegemea upande wowote katika diplomasia bado ni “jambo la kutia wasiwasi mkubwa.”

    Serikali ya Ethiopia na chama tawala katika eneo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo zimeshutumiana kuhusika na mashambulizi hayo, hali inayozua hofu ya kurejea kwa mapigano makubwa.

    Getachew Reda, waziri wa serikali na mshauri wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, amesema wapiganaji wa Tigray wamechukua udhibiti wa viwanja vya ndege vinavyodhibitiwa na serikali ya shirikisho huko Tigray, na wameanzisha mashambulizi katika maeneo jirani ya Afar na Amhara.

    Awali, mamlaka za Tigray zilisema vikosi vyao vimelazimika kuingia katika “vita vya kujihami.” Kauli hiyo ilitolewa baada ya kuripotiwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani huko Tigray.

    Vita vya miaka miwili huko Tigray vilimalizika mwaka 2022, lakini katika miezi ya hivi karibuni pande zote mbili zimekuwa zikishutumiana kwa kukiuka makubaliano ya amani.

    Vita hivyo vilikuwa miongoni mwa migogoro iliyosababisha vifo vingi zaidi katika karne hii. Mpatanishi wa Umoja wa Afrika alikadiria kuwa karibu watu 600,000 walifariki katika mzozo huo, uliosababisha eneo hilo kuingia katika hali mbaya ya kibinadamu inayokaribia kuwa janga la njaa.

    Soma Pia:

  5. Trump ampokea Xi Jinping Marekani huku mvutano kati ya mataifa hayo ukiendelea

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump amempokea Rais wa China Xi Jinping nchini Marekani kwa ziara ya siku tatu, huku viongozi hao wakitarajiwa kujadili masuala nyeti yanayoendelea kuathiri uhusiano kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani.

    Xi amewasili Washington katika ziara yake ya kwanza nchini Marekani baada ya takriban miaka mitatu.

    Trump amempokea Xi katika kituo cha kijeshi cha Joint Base Andrews, Maryland, katika hafla yenye heshima za kijeshi, ikiwemo muziki wa bendi ya kijeshi, mizinga na ndege ya kivita ya B1 iliyopita angani.

    Mazungumzo yao yanatarajiwa kugusa biashara, teknolojia, Taiwan na mzozo wa Iran, huku Washington na Beijing zikiwa bado zinakabiliwa na tofauti kubwa katika maeneo hayo.

    Wakati huo huo, Waziri wa Hazina wa Marekani Scott Bessent amesema Marekani na China zimekubaliana kuongeza muda wa makubaliano yao ya kusitisha vita vya kibiashara hadi Januari.

    Hata hivyo, matarajio ya kufikiwa kwa makubaliano makubwa zaidi katika ziara hiyo yanaonekana kuwa madogo, huku suala la Taiwan likiwa miongoni mwa mada ambazo Beijing inatarajiwa kulisisitiza.

    Kwa upande wake, Xi amesema Marekani na China zinapaswa kuwa washirika badala ya wapinzani, wakati viongozi hao wakijaribu kudhibiti tofauti zao katika biashara, teknolojia na masuala ya kimkakati.

    Ziara hiyo inafanyika wakati uhusiano kati ya Washington na Beijing ukiendelea kuwa muhimu kwa uchumi wa dunia, huku maamuzi ya viongozi hao yakitarajiwa kuwa na athari zaidi ya mataifa hayo mawili.

    Soma Pia:

  6. Tetesi za soka Alhamisi: Barcelona yaondoa uwezekano wa kumsajili Alvarez

    c

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Barcelona imeondoa uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Argentina, Julian Alvarez, kutoka Atletico Madrid katika dirisha la usajili la Januari. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 anasubiri kuona iwapo Paris St-Germain au Arsenal itawasilisha ofa ya kumsajili, au kama ataamua kubaki Atletico Madrid.(Fichajes - in Spanish)

    Liverpool haiko tayari kumuuza kiungo wa Ujerumani, Florian Wirtz, mwenye umri wa miaka 23, kwenda Bayern Munich katika dirisha la usajili la Januari. Hata hivyo, mabingwa hao wa Ujerumani wanaweza kujaribu kumsajili msimu ujao wa kiangazi iwapo winga wa Ufaransa, Michael Olise, mwenye miaka 24, atakataa kusaini mkataba mpya. (Christian Falk - Bayern Insider/Bild)

    Chelsea imewaweka kiungo wa Bournemouth, Alex Scott, mwenye miaka 23, pamoja na kiungo wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Adam Wharton, mwenye miaka 22, kama walengwa wake wakuu katika eneo la kiungo. Klabu hiyo ya London Magharibi haionyeshi tena nia ya kumsajili kiungo wa Monaco na Senegal, Lamine Camara, mwenye miaka 22.(CaughtOffside, external)

    Aston Villa inataka kumpa kiungo wa Argentina, Emi Buendia, mwenye miaka 29, mkataba mpya kama zawadi kwa kiwango bora alichoonyesha hivi karibuni. (Mail)

    Beki wa kushoto wa England, Luke Shaw, mwenye miaka 31, anaweza kuondoka Manchester United baada ya mkataba wake wa sasa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao. (Teamtalk)

    Udinese inatarajiwa kumsajili beki wa Austria, David Alaba, mwenye miaka 34, ambaye aliondoka Real Madrid msimu huu wa kiangazi. (Fabrizio Romano)

    Pia unaweza kusoma:

  7. Iran yasema haitakubali kutishwa na Marekani, lakini iko tayari kwa mazungumzo

    f

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema kuwa Iran haitawahi “kupiga magoti” baada ya karibu miezi saba ya vita dhidi ya Marekani na Israel, huku akisisitiza kuwa Tehran iko tayari kufikia suluhisho la kidiplomasia la mzozo huo.

    Akijibu tishio la Rais wa Marekani Donald Trump kwamba Jamhuri ya Kiislamu inaweza “kuangamizwa kabisa” iwapo makubaliano hayatapatikana hivi karibuni, Pezeshkian aliliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa:

    “Upinzani wa wananchi wa Iran utaongezeka zaidi mbele ya vikwazo, kuongezwa kwa shinikizo na vitisho.”

    Pezeshkian pia alisisitiza kuwa makubaliano yoyote lazima yajumuishe kusitishwa kwa kile Iran inachokitaja kuwa ni kizuizi cha Marekani kinachozuia meli za Iran kutumia njia muhimu ya majini katika Ghuba.

    “Haikubaliki kwamba kila mtu anufaike na Mlango-Bahari wa Hormuz huku sisi tukinyimwa fursa ya kuutumia,” alisema.

    Hakukuwa na tamko la haraka kutoka upande wa Marekani, ambao ujumbe wake ulitoka katika ukumbi wa Baraza Kuu mwanzoni mwa hotuba ya Pezeshkian.

    Soma Zaidi:

  8. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja ya 24/09/2026.