Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Bunge la Marekani laidhinisha mswada wa vikwazo dhidi ya Iran na Urusi

Mswada huo, unaofahamika kama Sheria ya Lindsay O. Graham ya Vikwazo dhidi ya Urusi na Iran, ulipitishwa Jumatano kwa kura 262 dhidi ya 159.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

  1. Mwanahabari aliyetekwa Afrika Kusini apatikana amefariki

    Salamu za rambirambi zinaendelea kumiminika kufuatia kifo cha mtangazaji mkongwe wa michezo wa Afrika Kusini, Owen Ndlovu, ambaye alipatikana amefariki dunia saa chache baada ya kutekwa nyara wakati wa tukio la uporaji wa gari karibu na Johannesburg.

    Kwa mujibu wa polisi, Ndlovu, mtangazaji wa zamani wa Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC), alitekwa Jumanne alipokuwa akimchukua mkewe kutoka kanisani katika eneo la Katlehong.

    Mwili wake ulipatikana na wakazi asubuhi ya Jumatano, huku mashahidi wakisema ulikuwa na majeraha ya risasi.

    Polisi wameanzisha msako wa watu watatu wanaoshukiwa kuhusika na tukio hilo na wanaendelea kuchunguza mazingira ya mauaji hayo.

    Kisa hicho kwa mara nyingine kimeibua mjadala kuhusu viwango vya juu vya uhalifu wa vurugu vinavyoendelea kuikabili Afrika Kusini.

    Zaidi soma hapa:

  2. Marekani yapandisha riba kwa mara ya kwanza ndani ya miaka mitatu

    Benki Kuu ya Marekani (Federal Reserve) imeongeza kiwango chake cha riba kwa pointi 25 za msingi hadi kufikia kati ya asilimia 3.75 na 4.00, hatua inayoashiria kuongezeka kwa wasiwasi kuhusu mfumuko wa bei unaoendelea kuisumbua nchi hiyo.

    Uamuzi huo ulipitishwa kwa kauli moja na wajumbe wote 12 wa kamati ya sera za fedha ya benki hiyo, ukiwa ni ongezeko la kwanza la riba katika kipindi cha miaka mitatu.

    Ongezeko la viwango vya riba linatarajiwa kuongeza gharama za mikopo kwa kaya na wafanyabiashara, hali ambayo inaweza kupunguza matumizi makubwa ya fedha na uwekezaji. Wataalamu wa uchumi wanasema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kudhibiti mfumuko wa bei, ingawa pia inaweza kuathiri kasi ya ukuaji wa uchumi na uundaji wa ajira.

    Hatua hiyo imekuja wakati Rais Donald Trump akiendelea kusisitiza umuhimu wa kupunguzwa kwa viwango vya riba ili kuchochea shughuli za kiuchumi. Tofauti hiyo ya msimamo kati ya Ikulu ya White House na Benki Kuu imeibua mjadala kuhusu uhuru wa taasisi hiyo katika kufanya maamuzi ya sera za fedha.

    Wakati huo huo, vita vinavyoendelea na Iran vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizoongeza shinikizo la kiuchumi. Federal Reserve ilieleza awali kuwa kupanda kwa bei za nishati, gharama za uzalishaji na usafirishaji kulichangiwa na usumbufu wa usafiri katika Mlango wa Hormuz pamoja na athari za mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati.

    Kutokana na hali hiyo, wananchi wa Marekani wanakabiliwa na changamoto ya kupanda kwa gharama za maisha, ikiwemo bei ya mafuta na gharama za kukopa fedha.

    Maelezo zaidi:

  3. Wahouthi wachapisha picha za ndege ya Saudia waliyodai kuidungua

    Kundi la Wahouthi nchini Yemen limesema ndege za kijeshi za Saudi Arabia zimetekeleza mashambulizi 40 katika majimbo matatu ndani ya saa 24 zilizopita, huku mapigano kati ya pande hizo yakiendelea kuongezeka.

    Katika taarifa, kundi hilo lilidai kutekeleza mashambulizi mawili dhidi ya malengo nchini Saudi Arabia. Wahouthi walisema walishambulia miundombinu ya kampuni ya mafuta ya Aramco mjini Yanbu kwa kutumia makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani, wakidai shambulio hilo lilisababisha moto mkubwa na uharibifu wa mali.

    Kundi hilo pia lilisema lililenga Kituo cha Jeshi la Anga cha Khamis Mushait kwa makombora ya balistiki, likidai mashambulizi hayo yalifanikiwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.

    Siku ya Jumatano, Wahouthi walitangaza kuwa walidungua ndege ya kivita ya Saudi Arabia aina ya F-15 katika anga ya jimbo la Marib. Msemaji wa kundi hilo, Brigedia Jenerali Yahya Saree, alisema ndege hiyo ilitunguliwa kwa kombora la kutoka ardhini kwenda angani lililotengenezwa ndani ya Yemen wakati ikishiriki operesheni za kijeshi katika eneo hilo.

    Baadaye, Wahouthi walichapisha video walizodai zinaonyesha tukio la kudunguliwa kwa ndege hiyo na mabaki yake baada ya kuanguka.

    Kwa upande mwingine, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulisema ulidungua ndege isiyo na rubani iliyokuwa imerushwa na Wahouthi kuelekea mji mtakatifu wa Makka. Hata hivyo, Wahouthi walikanusha madai hayo na kuyataja kuwa hayana ukweli.

    Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametoa wito wa kuanzishwa kwa mazungumzo yenye dhamira ya dhati kati ya pande zinazohasimiana, akisisitiza kuwa hatua za kijeshi pekee haziwezi kuleta suluhu ya kudumu kwa mgogoro unaoendelea nchini Yemen.

    Unaweza kusoma:

  4. Wanadiplomasia wa Marekani wakutana na wawakilishi wa Wahouthi Oman -ripoti

    Wanadiplomasia wa Marekani walikutana na wawakilishi wa kundi la Wahouthi mjini Muscat, Oman, mwishoni mwa wiki iliyopita kujadili hali ya usalama katika Bahari ya Shamu na Mlango-bahari wa Bab al-Mandab, kwa mujibu wa ripoti ya Axios.

    Mazungumzo hayo yalifanyika kwa ushirikiano wa serikali ya Oman na yalilenga kudumisha makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya pande hizo pamoja na kuhakikisha usalama wa usafiri wa meli katika njia hiyo muhimu ya biashara.

    Mkutano huo unafanyika wakati Wahouthi wakiongeza ushawishi wao katika Bab al-Mandab, huku Marekani ikiwa mbioni kuzuia usumbufu wa usafirishaji na athari zake kwa soko la nishati, bila kuingia katika operesheni za kijeshi za pamoja na Saudi Arabia.

    Soma pia:

  5. Tetesi za Soka Ulaya Alhamisi: Luke Shaw kuondoka United?

    Klabu ya Arsenal imeripotiwa kukataa ofa zilizowasilishwa kwa ajili ya kumchukua kwa mkopo mshambuliaji wake .

    Taarifa zinaeleza kuwa Luton Town, inayoshiriki League One, iliwasiliana mara kadhaa na Arsenal ikitaka kumnasa nyota huyo wa England mwenye umri wa miaka 16 kwa mkataba wa mkopo, lakini ombi hilo halikupata kibali kutoka kwa klabu hiyo ya London.

    Beki wa England Luke Shaw huenda akaondoka Manchester United mwishoni mwa msimu ujao, hakuna dalili za mazungumzo kuhusu kuongeza mkataba wake kwa sasa.

    Wakati huo huo, kiungo wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 17, Noah Ajayi, anakaribia kusaini mkataba wake wa kwanza wa kulipwa na Manchester United.

    Arsenal, Brighton na Aston Villa zinaendelea kumfuatilia kiungo wa Austria mwenye umri wa miaka 17, Luca Weinhandl wa Sturm Graz, ambaye anaripotiwa kuwa anaweza kupatikana kwa ada ya takriban pauni milioni 17.

    Liverpool inafikiria kumsajili mwezi Januari kiungo wa Monaco na timu ya taifa ya Senegal, Lamine Camara (22), baada ya kukosa kuhamia Chelsea siku ya mwisho ya usajili.

    Tottenham Hotspur ni klabu ya karibuni zaidi kuhusishwa na mshambuliaji wa Argentina Mauro Icardi (33), ambaye kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kuondoka Galatasaray mwezi Julai.

    Arsenal pia inaendelea kufuatilia hali ya winga wa Brazil Rodrygo (25) aliyejeruhiwa akiwa Real Madrid, baada ya kuonyesha nia ya kumsajili wakati wa usajili la majira ya kiangazi.

    Mshambuliaji chipukizi wa England Vincent Joseph (16) amethibitisha kuondoka Liverpool, huku akitarajiwa kujiunga na Arsenal.

    Leeds United haitaharakisha uamuzi wa kugeuza mkopo wa mshambuliaji wa Eintracht Frankfurt, Jean-Matteo Bahoya (21), kuwa mkataba wa kudumu, licha ya kuwa na kipengele cha kumnunua kwa pauni milioni 19.7.

    Aliyekuwa mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya Ufaransa, Anthony Martial (30), anatarajiwa kujiunga na klabu ya Malaga nchini Hispania kama mchezaji huru.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Muisrael ahukumiwa miaka 13 Jela kwa ujasusi wa Iran

    Mahakama nchini Israel imemhukumu kifungo cha miaka 13 jela mwanaume mwenye umri wa miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa niaba ya Iran.

    Mwendesha mashtaka alieleza kuwa mtuhumiwa Alexander Granevsky alihusika katika shughuli za kukusanya na kusambaza taarifa kwa mawakala wa Iran, jambo ambalo mahakama ilitaja kuwa lilihatarisha usalama wa taifa la Israel

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, hukumu hiyo ni miongoni mwa adhabu kali zaidi kuwahi kutolewa nchini humo katika kesi zinazohusiana na shughuli za ujasusi kwa niaba ya Iran.

    Waendesha mashtaka walisema Granevsky alitekeleza misheni kadhaa baada ya kuwasiliana na mtu aliyedaiwa kuwa wakala wa Iran kupitia programu ya Telegram, akiahidiwa malipo ya fedha kwa kazi alizopewa.

    Mahakama ilimpata na hatia ya kuandika kaulimbiu za kupinga serikali katika maeneo mbalimbali kwa kutumia rangi ya dawa ya kupuliza, kuchoma moto magari tisa, pamoja na kufuatilia eneo la makazi la Benny Gantz, aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Israel na Waziri wa Ulinzi.

    Pia alihukumiwa kwa kupiga picha za maeneo nyeti, yakiwemo miundombinu ya kuzalisha umeme, na kuwasilisha taarifa hizo kwa mawasiliano yake wa Iran.

    Mamlaka za Israel zimekuwa zikitahadharisha kuhusu kile zinachodai ni juhudi za Iran za kuwatumia raia wa Israel kukusanya taarifa za kiintelijensia na kutekeleza vitendo vya hujuma ndani ya nchi.

    Hukumu ya Granevsky inaonekana kuashiria msimamo mkali wa Israel dhidi ya vitendo vinavyohusisha ushirikiano na mataifa yanayoonekana kuwa tishio kwa usalama wa taifa.

    Soma zaidi:

  7. Bunge la Marekani laidhinisha mswada wa vikwazo dhidi ya Iran na Urusi.

    Bunge la Wawakilishi la Marekani limepitisha mswada mpya unaopanua wigo wa vikwazo dhidi ya Urusi na Iran, hatua inayolenga kuongeza shinikizo kwa mataifa hayo kutokana na shughuli zake za kiuchumi na kijeshi.

    Mswada huo, unaofahamika kama Sheria ya Lindsay O. Graham ya Vikwazo dhidi ya Urusi na Iran, ulipitishwa Jumatano kwa kura 262 dhidi ya 159, baada ya awali kupitishwa na Seneti mwezi Agosti kwa kura 86 dhidi ya 11. Sasa unasubiri kutiwa saini na Rais wa Marekani, Donald Trump, ili kuwa sheria.

    Chini ya sheria hiyo, Marekani itaweza kuweka vikwazo dhidi ya maafisa wa Urusi, taasisi za kifedha, benki pamoja na sekta za nishati na ulinzi za nchi hiyo.

    Aidha, mswada huo unalenga kile kinachoitwa “shadow fleet” au meli zinazotumiwa kusafirisha mafuta ya Urusi kwa lengo la kukwepa vikwazo vya kimataifa.

    Sheria hiyo pia itampa Rais wa Marekani mamlaka ya kuweka ushuru wa hadi asilimia 100 kwa nchi zinazotambuliwa kuwa wanunuzi wakubwa wa mafuta na gesi kutoka Urusi.

    Kwa upande wa Iran, mswada huo unapanua vikwazo vinavyohusiana na ushirikiano wake na Urusi, hususan katika maeneo ya kijeshi.

    Vilevile, sheria hiyo itaongeza muda wa uhalali wa Sheria ya Vikwazo dhidi ya Iran ya mwaka 1996 kwa kipindi cha miaka mitano zaidi, kuanzia mwaka 2026 hadi 2031. Hatua hiyo inalenga kuendelea kudumisha mfumo wa kisheria wa vikwazo uliopo.

    Hata hivyo, mswada huo haujaweka orodha mpya ya watu binafsi au makampuni yatakayowekewa vikwazo. Badala yake, unatoa msingi wa kuchukuliwa hatua dhidi ya taasisi na makampuni ya Iran yatakayobainika kushiriki katika ushirikiano wa kijeshi na Urusi.

    Maelezo zaidi:

  8. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.