DRC: Tshisekedi adai kesi dhidi ya familia yake Ubelgiji ni njama ya kumharibia sifa

Chanzo cha picha, AFP
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, amesema kesi inayowakabili baadhi ya wanafamilia wake nchini Ubelgiji ni kampeni ya kumchafua inayoratibiwa na wapinzani wake, akiiita njama ya kihalifu inayolenga kuharibu sifa yake.
Kwa mujibu wa Radio Okapi, Tshisekedi alitoa kauli hiyo alipokutana na raia wa Congo wanaoishi nchini Urusi.
Kituo hicho cha redio kilinukuu mahojiano aliyofanya kwa lugha ya Lingala, ambayo baadaye yalichapishwa kwenye akaunti ya Ofisi ya Rais katika mtandao wa X.
Tshisekedi amesema wapinzani wake waligeukia familia yake baada ya kuona kuwa alikuwa na uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wananchi.
Amesema awali walimtuhumu kutumia vibaya fedha za serikali kwa safari, lakini Benki Kuu ya Congo ilieleza kuwa fedha hizo zilikuwa zimetengwa kwenye bajeti.
Rais huyo aliwashutumu wakili aliyemtaja kuwa bandia na aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila, kwa kushirikiana katika kile alichokiita njama ya kumfikia kupitia familia yake.
Alisema: “Kisha waliamua kuishambulia familia yangu. Waliungana na wakili bandia ambaye amekuwa akishirikiana na Wanyarwanda kwa miaka 30, pamoja na mtu tuliyemwondoa madarakani, ili kuihujumu familia yangu wakitarajia kuwa hilo pia litaniathiri.”
Akizungumzia uchunguzi unaoendelea kuhusu kesi hiyo, Tshisekedi amesema hadi sasa hakuna ushahidi muhimu uliojitokeza kuhusu fedha zinazotiliwa shaka au vitu vilivyokamatwa wakati wa upekuzi.
Amesema bado anasubiri kufahamishwa ni nini hasa kilichopatikana katika upekuzi huo.
Tshisekedi amesema tayari ameunda timu ya mawakili ili kukabiliana na madai hayo kupitia njia za kisheria.
“Tumeajiri timu ya mawakili. Tutawajibu wanaotushutumu,” alisema.
Rais huyo amekanusha tuhuma zinazohusisha baadhi ya wanafamilia wake na uchimbaji haramu wa madini ya thamani katika eneo la Katanga.
Badala yake, amedai kuwa watu waliohusika na uporaji wa rasilimali za asili katika eneo hilo wanajulikana, akiwataja aliyekuwa rais Joseph Kabila na Moïse Katumbi, gavana wa zamani wa Katanga ambaye sasa ni mwanasiasa wa upinzani anayeishi uhamishoni.
Kauli hizo zinatolewa wakati kesi dhidi ya baadhi ya wanafamilia wa Tshisekedi ikiendelea kuzua mjadala nchini DRC na kuongeza mvutano katika uhusiano kati ya Kinshasa na Brussels.
Unaweza pia kusoma:



























