Moto wafufua mjadala wa CCTV mashuleni, usalama kwanza au faragha?

Chanzo cha picha, MTANDAONI
Katika siku za hivi karibuni, kisa cha kamera fiche ya CCTV ilivyonasa wanafunzi saba wakishukiwa kupanga njama ya kuchoma bweni iliyoua wanafunzi 16 katika shule ya upili ya wasichana ya Utumishi Academy nchini Kenya kimeibua mjadala mkali.
Baadhi wameeleza kuwa video hii ilileta ufunuo wa kilichosababisha moto huo huku wengine wakihisi kwamba kamera fiche za CCTV kuwekwa kwa bweni ni kuingilia faragha ya wanafunzi wa kike.
Hata hivyo, Mtaalamu wa masuala ya faragha ya data Philip Kisaka anasema kuna maeneo ambayo mtu anatarajiwa kuwa na faragha kamili, kama vile vyumba vya kulala, bafu, msalani na vyumba vya kubadilishia nguo. Katika maeneo hayo, matumizi ya CCTV yanaweza kukiuka haki ya faragha inayolindwa na Katiba ya Kenya pamoja na Sheria ya Ulinzi wa Data.
"Msingi mkuu ni kwamba lazima kuwe na sababu halali ya kutumia kamera. Huwezi kufunga CCTV mahali ambapo watu wanatarajia kufanya shughuli zao binafsi bila kufuatiliwa," anasema Philip.
Akiiambia BBC Swahili kuwa iwapo wazazi wa shule ya Utumishi waliridhia na wanafunzi walijua kuna kamera fiche haiwezi kuchukuliwa faragha yao iliingiliwa.
Faragha ya wanafunzi wa Utumishi ilikiukwa?

Chanzo cha picha, Getty Images
''Pia vigezo vingine vitatumika kujua haki ya faragha ya wanafunzi ilikiukwa ni kubainishwa kuwa matumizi ya CCTV katika bweni hilo yalikuwa yanalenga nini'', anaendelea kueleza.
Hii ndiyo kanuni inayojulikana kama purpose limitation, yaani taarifa zinapaswa kukusanywa kwa sababu maalum na kutotumika nje ya kusudi hilo. Hili limeainishwa kutoka kwa sheria ya ulinzi wa data 2019.
"CCTV ni shahidi wa kimya, haiwezi kuzuia tukio kutokea, lakini inaweza kusaidia kubaini ukweli baada ya tukio kutokea'', anasema mtaalamu wa faragha ya data Philip Kisaka.
Kwa mujibu wa katiba ya Kenya kifungu cha 31 kinasema kuwa kila raia ana haki ya kuwa na faragha hasa maeneo binafsi na mawasiliano binafsi kuwekwa wazi.
Baada ya tukio hilo waziri wa usalama wa ndani Kenya Kipchumba murkomen aliwashauri wasimamizi wa shule za bweni kufunga CCTV na ziwe na wafanyakazi wa kufuatilia kinachoendelea kama njia ya kiusalama.
''Ni muhimu kwa wasimamizi wa shule kuchukua hatua na kufunga kamera fiche ambazo zinafuatiliwa ili kuepuka majanga shuleni'' alisema Murkomen akirejelea mkasa wa moto katika shule ya Utumishi.
Hata hivyo kamishna wa data za faragha ameonya kuwa kuwekwa kwa CCTV kwa mabweni inaibua kuingilia faragha ya wanafunzi.
Je, mtu anaweza kurekodiwa bila ridhaa yake?

Jibu linategemea mazingira.
Ikiwa kamera imewekwa katika eneo la biashara au sehemu ya umma kwa sababu za usalama, si lazima kila mtu apewe ruhusa binafsi kabla ya kurekodiwa. Hata hivyo, sheria inataka watu wafahamishwe kuwa eneo hilo lina CCTV.
Ndiyo maana katika majengo mengi, maduka na ofisi utaona mabango yanayoeleza kuwa eneo hilo linafuatiliwa kwa kamera.
"Mtu anapoingia katika eneo ambalo limetangazwa wazi kuwa lina CCTV, mara nyingi inachukuliwa kuwa amefahamu uwepo wa kamera hizo na ameridhia," anasema mtaalamu huyo.
Iwapo utajipata katika eneo ambalo halina ilani ya kufungwa kwa kamera fiche kama vile vyumba vya kulalia, mtaalam anasema kuwa una haki ya kushtaki mmiliki wa eneo hilo na kulipwa fidia.
Rekodi za CCTV zinapaswa kuhifadhiwa kwa muda gani?
Sheria ya Kenya haijaweka muda maalum wa kuhifadhi rekodi za CCTV.
Badala yake, inataka rekodi hizo zihifadhiwe kwa muda unaofaa kulingana na sababu ya kuzikusanya.
Kwa mfano, ikiwa rekodi za video zinahitajika kusaidia uchunguzi wa tukio la uhalifu, zinaweza kuhifadhiwa hadi uchunguzi au kesi husika itakapokamilika.
Baada ya hapo, mmiliki wa mfumo anatakiwa kuhakikisha taarifa hizo hazihifadhiwi bila sababu ya msingi.
Tofauti kati ya CCTV za nyumbani na za umma
Sheria inaweka tofauti kati ya kamera zinazotumiwa nyumbani na zile zinazotumiwa katika biashara.
Kamera za nyumbani zinapaswa kuelekezwa ndani ya eneo la mwenye nyumba na zisirekodi maeneo ya umma au mali za majirani bila sababu halali.
''Sheria inasema kamera za nyumbani ukiweka kwa lango hazipaswi kumulika hata sehemu ndogo ya umma, ukifanya hivyo unakiuka sheria'', anasema.
Kwa upande wa biashara, matumizi ya CCTV yanaruhusiwa zaidi kwa madhumuni ya usalama, lakini lazima yaambatane na taarifa za kuwajulisha watu wanaoingia katika eneo husika.
''Lazima uweke ilani kuwa mazingira haya yanamulikwa na kamera fiche'', asema mtaalamu wa data za faragha.
Namna kamera za siri zinavyofanya kazi

Kamera fiche za CCTV kama jina lake huwekwa mahali sio rahisi kwa macho ya binadamu kuona.
Inatumika kama macho ya pili ya binadamu yasio fumba ima usiku au mchana.
Lakini hufanya vipi kazi hiyo, kwa kweli ni teknolojia ya akili unde AI.
Kamera hufanya kazi kwa kunasa mwanga kupitia lenzi, kisha kuugeuza kuwa mawimbi ya video ya kidijitali kwa kutumia kihisi picha (image sensor).
Taarifa hizo husindikwa na kuhifadhiwa au kuonyeshwa moja kwa moja kwa mtumiaji.
Baadhi ya aina zina vitu vya ziada kama Bluetooth kwa mawasiliano au muziki, maiki kwa ajili ya kurekodi sauti, na lenzi 'polarized lenses' kwa ajili ya jua.
Kama sehemu ya mfumo wa usalama, kamera husaidia kuzuia uhalifu, kurekodi ushahidi unaoweza kutumika baadaye na kutoa tahadhari za haraka pale shughuli zisizo za kawaida zinapotokea.
Kwa nini video za CCTV huonekana nyeusi na nyeupe usiku?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mojawapo ya mambo ambayo watu wengi walijiuliza walipoona rekodi za CCTV picha za usiku wa manane za bweni lililotoketea Kenya zilionekana katika rangi za nyeusi, nyeupe na kijivu badala ya rangi halisi.
Jibu lake liko katika teknolojia inayotumika na kamera hizo.
Wataalamu wa teknolojia ya usalama wanasema kuwa kamera nyingi za CCTV hubadilika moja kwa moja na kuingia katika mfumo wa kuona usiku pale kiwango cha mwanga kinapopungua.
Katika mazingira ya giza, kamera huwasha miale maalum ya infraredi ambayo haiwezi kuonekana kwa macho ya binadamu. Miale hiyo huisaidia kamera "kuona" vitu vilivyopo hata wakati hakuna mwanga wa kutosha.
Badala ya kurekodi rangi, kamera hujikita katika kupima kiasi cha mwanga kinachorejea kutoka kwenye vitu vilivyo mbele yake. Matokeo yake ni picha za rangi moja, ambapo sehemu zenye mwanga mwingi huonekana nyeupe, huku maeneo yenye mwanga mdogo yakionekana katika vivuli vya kijivu na nyeusi.
Teknolojia hiyo ndiyo iliwezesha kamera za usalama kurekodi matukio usiku na kusaidia uchunguzi wa moto ulioteketeza wanafunzi 16 na wengine kujeruhiwa vibaya.
Kwa hivyo, video za CCTV zinapoonekana nyeusi na nyeupe usiku, si kwa sababu kamera imeharibika au imepoteza uwezo wa kurekodi rangi. Ni kwa sababu imehamia katika mfumo maalum wa kuona usiku unaotegemea mwanga wa infraredi ili kuendelea kurekodi katika mazingira yenye mwanga hafifu.
Namna ya kujilinda usirekodiwa kwa siri
Kuna mbinu mbalimbali zinazoweza kusaidia mtu kujiulinda dhidi ya kamera za siri. Kwanza, kutumia simu kupitia Guided Access na Accessibility Shortcut, pamoja na kuchagua Magnifier, inaweza kusaidia kugundua kamera zilizofichwa ndani ya chumba.
Bonyeza mara tatu kwenye sehemu za kuzimia husaidia kugundua vifaa vya 'elektroniki vilivyojificha kama kamera za simu, kamera za miwani na nyingine utakapokuwa mazingira ya ndani.
Pili, ni muhimu kuwa makini na mazingira unayokuwa. Vyumba vya hoteli, ofisi ndogo, au vyumba vya kubadilisha nguo vinaweza kuwa na kamera. Angalia nyuso zisizo za kawaida, vifaa vinavyobadilika mara kwa mara, na vitu vya elektroniki visivyojulikana. Mbinu hii husaidia kupunguza hatari ya kurekodiwa bila ridhaa.
Tatu, angalia vitaa, au kitaa kinachowakawaka, kamera nyingi za kificho zina aina hii za taa ambazo kwa macho ya haraka haraka huwezi kuona.
'Sheria hazitoshi kutokana na teknolojia ya kisasa'
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, sheria zilizopo zimetoa msingi mzuri wa kulinda haki ya faragha.
Hata hivyo, maendeleo ya teknolojia kama akili unde (AI) na teknolojia za kutengeneza video bandia zinazojulikana kama deepfake yanaibua changamoto mpya.
"Teknolojia inabadilika kwa kasi kubwa. Hivyo sheria nazo zinahitaji kuendelea kuboreshwa ili ziweze kukabiliana na mazingira mapya na kuhakikisha haki za wananchi zinaendelea kulindwa," anasema.
Katika enzi ambayo kamera zipo karibu kila mahali, mjadala hauhusu tu usalama. Unahusu pia namna ya kupata uwiano kati ya kulinda jamii dhidi ya uhalifu na kulinda haki ya kila mtu ya kuwa na faragha.













