'Sikujua nilikuwa na upungufu wa vitamini D hadi nilipozirai kazini'

Chanzo cha picha, Saskia Reeves-Priestley
Msichana mwenye umri wa miaka 23, Saskia Reeves-Priestley, alikuwa kazini, ghafla alianguka na kupoteza ufahamu.
"Nilianza kuhisi kizunguzungu, kichefuchefu, moyo kwenda mbio na mwili kuwa na joto sana," anasema.
Saskia, ambaye ni mwalimu wa wanafunzi wenye mahitaji maalum ya kielimu, alikuwa mchezaji mahiri wa soka, akicheza kama golikipa mara nne kwa wiki. Alikuwa akijihisi yuko na afya njema na sawa kimwili.
Ingawa dalili alizokuwa nazo hazihusiani moja kwa moja na upungufu wa vitamini D, wakati mwingine alikuwa anahisi kila kitu hakiko sawa.
Alifanya vipimo vya damu ambavyo baadaye vilionyesha kuwa kiwango chake cha vitamini D mwilini kilikuwa chini sana, kiasi kwamba kilikuwa karibu kutokuwepo kabisa.
Nchini Uingereza, visa vya upungufu wa vitamini D vimeongezeka miongoni mwa wasichana na wanawake vijana.
Kulingana na takwimu za Utafiti wa Kitaifa wa Lishe na Ulaji mwaka uliopita karibu robo ya vijana wenye umri wa miaka 11 hadi 18 waligunduliwa kuwa na upungufu wa vitamini D.
Vitamini D hupatikana kupitia vyakula tunavyokula, kama vile samaki wenye mafuta mengi na nyama, au kwa kutumia virutubisho.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya vitamini hiyo huzalishwa na mwili wenyewe pale miale ya jua kutoka kwenye mwanga wa jua inapogusa ngozi. Upungufu wa mwanga wa jua, kutegemea eneo la kijiografia unaloishi au msimu wa mwaka, na wakati mwingine, hupunguza uwezo wa mwili kuzalisha vitamini hiyo.
Kufunika baadhi ya sehemu za mwili na kutumia mafuta ya kujikinga na miale ya jua au sunscreen pia kunaweza kuathiri uzalishaji wa vitamini D, licha ya hatua hizo kuwa na faida katika kulinda ngozi.
Watu wenye ngozi nyeusi huhitaji kupata mwanga wa jua wenye nguvu zaidi ili kuzalisha kiwango sawa cha vitamini D ikilinganishwa na watu wenye ngozi nyepesi.
Madaktari huwa hawafanyi vipimo vya damu mara kwa mara ili kubaini upungufu wa vitamini D. Hata hivyo, wanaweza kumpa mgonjwa virutubisho vya vitamini hiyo iwapo atakuwa na wasiwasi kuwa yuko katika hatari kubwa ya kukumbwa na upungufu huo.
Kwa nini vitamini D ni muhimu?
Vitamini D husaidia kudumisha afya ya mifupa, meno na misuli kwa kudhibiti virutubisho muhimu mwilini.
Hata hivyo, si kila mtu hupata kiwango cha kutosha cha vitamini, jambo linaloweza kusababisha upungufu wa vitamini D na matatizo mbalimbali ya kiafya.
Dalili zake ni zipi na zinaathiri vipi maisha ya kila siku?
Upungufu wa vitamini D unahusishwa na ugonjwa wa mifupa unaojulikana kama rickets kwa watoto wachanga na wadogo.
Kwa watu wazima, husababisha hali inayofanana ya kudhoofika kwa mifupa inayojulikana kama osteomalacia.
"Wanauita ugonjwa wa kimya," anasema Dkt Suma Uday, daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa homoni kwa watoto, ambaye anataka kuongeza uelewa kuhusu tatizo hilo.
Anaonya kuwa upungufu wa vitamini D kwa vijana na watu wazima ni vigumu kugundua, na unaweza usitambuliwe au ukachanganywa na magonjwa mengine.
Miongoni mwa dalili zake ni uchovu wa mara kwa mara pamoja na maumivu ya viungo na mifupa.
Dkt Uday anasema,"Kimsingi, upungufu huu hudhoofisha mifupa taratibu bila mtu kutambua, na kuifanya iwe laini na rahisi kuvunjika."

Chanzo cha picha, Amaka Osu
Amaka alikuwa akiandaa chakula cha jioni katika chumba chao cha wanafunzi wa chuo kikuu jijini Liverpool, alipoanza kutetemeka.
"Kwa kweli sikuwa na uwezo wa kuona vizuri kilichokuwa mbele yangu," anasema Amaka.
Mwenzake aliyekuwa anaishi naye, alimpeleka hospitalini.Baadaye,mwenzake pia aligundulika kuwa na upungufu wa vitamini D.
Mbali na kujihisi mchovu, anasema hakuwa na dalili nyingine zozote.
"Mimi ni mwanafunzi wa miaka 21. Nina kazi na masomo ya chuo kikuu, kwa hiyo huwa ninahisi uchovu karibu kila wakati," anaelezea.
Anakumbuka mama yake pia aliwahi kukumbwa na upungufu wa vitamini D, lakini hakutambua kuwa hali hiyo ingeweza kumpata yeye pia.
Baada ya kuanza kutumia virutubisho vya vitamini D, Amaka anasema anajihisi vizuri zaidi. Hata hivyo, bado ana hofu kuwa hali hiyo inaweza kujirudia.
"Ilikuwa hali ya kutisha na sitaki kupitia hali hiyo tena," anaelezea Amaka.
Upungufu wa vitamini D kwa wasichana unaweza kudumu maisha yote
Dkt Uday ameungana na madaktari na wataalamu wengine wa taaluma kuunda kundi linaloitwa ACT NOW Vitamin D, ambalo linatoa wito wa kuongeza kiwango cha chini cha vitamini D kinachotumika kumtambua mtu kuwa na upungufu wa vitamini hiyo.
Anasema hatua hiyo itasaidia kuwagundua watu wengi zaidi wenye viwango vya chini vya vitamini D na kutoa picha sahihi zaidi ya ukubwa wa tatizo hilo.
Pia, kulingana naye,kampeni hiyo itawawezesha madaktari kuanza kutoa matibabu mapema zaidi kwa watu wenye upungufu huo.
Dkt Uday anaonya kuhusu uwezekano wa wanawake kukumbwa na upungufu wa vitamini D katika hatua mbalimbali za maisha yao, kuanzia kipindi cha ujana, wakati wa ujauzito, hadi kwa watoto wanaozaliwa.
"Iwapo hutarekebisha hali hiyo tangu mwanzo kabisa," anasema, "itaathiri vizazi vingi."

Chanzo cha picha, Liam Asman
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Inashtua sana," anasema Profesa Martin Hewison kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham.
Anasema kuwa licha ya kupita miaka 100 tangu vitamini D igunduliwe, ugonjwa wa riketi bado haujatokomezwa.
"Iwapo bado kuna visa vya ugonjwa wa riketi katika jamii, basi kuna uwezekano kuwa watu wengi zaidi wana upungufu wa vitamini D."
Anasema serikali inapaswa kuchunguza uwezekano wa kupanua mpango wa kuongeza vitamini kwenye vyakula wakati wa uzalishaji wake, utaratibu unaojulikana kama food fortification.
Nchi kama Canada na Uswidi tayari zina sera zinazolazimisha utaratibu huo kufanyika katika vyakula.
Nchini Uingereza, baadhi ya vyakula kama nafaka zinazoliwa wakati wa kifungua kinywa na vyakula vya kupaka kwenye mkate tayari huongezewa vitamini D, lakini utaratibu huo si wa lazima kwa wazalishaji.
Wakati wa miezi ya baridi, viwango vya vitamini D mwilini huanza kupungua.
"Huenda tukalazimika kukubali kuwa kwa baadhi ya makundi ya watu, matumizi ya virutubisho vya vitamini D yanapaswa kuwa sehemu ya kawaida ya maisha yao," anasema Hewison.
Kwa sasa, Saskia anaendelea kutumia virutubisho vya vitamini D mara kwa mara na amerejea uwanjani kucheza kama golikipa.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula na kuhaririwa na Ambia Hirsi
































