Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, unawezaje kukabiliana na upweke?
Haijalishi kama uko shuleni, chuoni au nyumbani, kuna nyakati ambazo unaweza kuhisi upweke.
Huenda ukahitaji rafiki wa kuzungumza naye au mtu wa kushirikiana naye katika shughuli za kila siku.
Wakati mwingine unaweza kulazimika kuhama nyumbani na kuanza maisha katika mazingira mapya. Hali hiyo inaweza kufanya iwe vigumu kupata marafiki wapya kwa haraka na kukusababishia hisia za upweke.
Hata hivyo, hauko peke yako. Watu wengi hupitia changamoto ya kujenga urafiki wanapoanza masomo chuoni, wanapohamia shule mpya au wanapoanza maisha katika makazi mapya.
Upweke ni nini?
Kwa mujibu wa Huduma ya Afya ya Taifa ya Uingereza (NHS), kila mtu hupitia upweke kwa namna tofauti, hivyo hupaswi kujilaumu kwa hisia unazopata. Wapo wanaohisi upweke mara chache, ilhali wengine hukumbwa na hali hiyo mara kwa mara.
NHS inaeleza kuwa upweke wa muda mrefu unaweza kuongeza hatari ya matatizo ya afya ya akili, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa ari ya kufanya shughuli mbalimbali, kuongezeka kwa wasiwasi na hata msongo mkubwa wa mawazo.
Aina za upweke
Upweke wa kihisia
Hali hii hutokea unapohisi kukosa uhusiano wa karibu wa kihisia na mwanafamilia au rafiki wa karibu.
Upweke wa kijamii
Ni hali ya kukosa marafiki au watu wenye maslahi na shughuli zinazofanana na zako.
Upweke wa kiuwepo
Hii ni hali ya kuhisi uko peke yako hata unapokuwa umezungukwa na watu wengi.
Jinsi ya kukabiliana na upweke
Ikiwa unahisi upweke, kuna hatua mbalimbali zinazoweza kusaidia kupunguza hisia hizo.
NHS inapendekeza:
- Dumisha mawasiliano na watu wengine.
- Jiunge na vikundi vya kijamii au shughuli za pamoja.
- Fanya shughuli unazozifurahia.
- Zungumza kuhusu hisia zako.
- Tafuta msaada kutoka kwa watu unaowaamini.
Madaktari wanasema kuwasiliana na wengine ni hatua muhimu, hata kama wakati mwingine unaweza kuhisi hakuna anayekuelewa. Kujenga mahusiano ya kweli kunaweza kusaidia kuboresha afya ya akili na ustawi wa jumla.
Daktari wa afya ya akili nchini Uingereza, Amir, anasema kwamba unapokuwa katika mazingira mapya, iwe ni shuleni, chuoni au mahali unapoishi, ni muhimu kujitahidi kuanzisha mazungumzo na watu wapya, kushiriki shughuli mbalimbali na kujenga mahusiano mapya.
Kwa mujibu wa Dkt Amir, hata kutumia muda mfupi mara kwa mara na mtu au kikundi hakumaanishi tayari mmekuwa marafiki wa karibu, lakini kuna manufaa kwa afya ya akili. Pia, kukutana na watu wapya nje ya mzunguko wako wa kawaida wa marafiki kunaweza kupunguza hisia za upweke.
End of Soma Zaidi:
Ushauri mwingine kutoka kwa wataalamu
Madaktari pia wanashauri:
- Jikubali jinsi ulivyo.
- Vuta pumzi kwa utulivu unapohisi msongo.
- Tabasamu mara kwa mara.
- Usijilazimishe kuhisi furaha kila wakati.
- Waoneshe wengine wema na huruma.
- Kumbuka thamani yako na uwezo ulionao.
Unapohitaji msaada
Daima zungumza na mtu kuhusu jambo lolote linalokusumbua au kukutia wasiwasi.
Unaweza kuzungumza na rafiki, mzazi, mlezi, mwalimu au mtu mwingine unayemwamini.
Iwapo unahitaji msaada, usisite kuutafuta. Na ikiwa unakabiliwa na changamoto za afya ya akili, ni muhimu kumwona mtaalamu wa afya au daktari ili kupata ushauri na matibabu yanayofaa.
Afrika ndiyo bara lenye upweke mkubwa zaidi duniani - WHO
Kwa mujibu wa ripoti ya mwezi Juni 2025 ya Shirika la Afya Duniani (WHO), Afrika ndiyo bara lenye kiwango kikubwa zaidi cha upweke duniani.
Takribani asilimia 24 ya watu barani humo walisema wamewahi kuhisi upweke, huku vijana wenye umri wa kati ya miaka 13 na 17 wakitajwa kuwa kundi lililoathirika zaidi.
Baada ya Afrika, kiwango cha juu cha upweke kilirekodiwa katika eneo la Mashariki ya Mediterania kwa asilimia 21, kikifuatiwa na Kusini Mashariki mwa Asia kwa asilimia 18. Ulaya ndiyo eneo lenye kiwango cha chini zaidi cha upweke, ambapo ni takribani asilimia 10 pekee ya watu walioripoti kuhisi hali hiyo.
Ripoti hiyo imechapishwa baada ya WHO kutangaza upweke kuwa changamoto kubwa ya afya ya umma duniani na kuanzisha tume ya kimataifa ya kuchunguza namna ya kuimarisha uhusiano wa kijamii na kupunguza athari za upweke.
Daktari Cleopa Mailu amesema dhana kwamba Afrika haina upweke imejengeka kutokana na mtazamo wa bara hilo kuwa na jamii zinazoshikamana. Hata hivyo, anasema hali hiyo imeanza kubadilika.
"Kumekuwa na mtazamo kwamba tumekuwa tukijiwasilisha kwa dunia kama bara lisilo na upweke wala kujitenga kijamii. Lakini hali hiyo siyo tena ilivyo," amesema.
Kwa muda mrefu, Afrika imekuwa ikitambulika kwa utamaduni unaoweka mbele mshikamano wa jamii na maslahi ya pamoja kuliko ya mtu binafsi. Hata hivyo, WHO inaeleza kuwa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yanaendelea kubadili hali hiyo.