Wanafunzi kadhaa wahofiwa kufariki katika moto wa bweni la shule Gilgil Kenya
Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya limesema limefika kwa tukio la moto ulioteketeza bweni katika Chuo cha Wasichana Utumishi kilichopo Gilgil, Kaunti ya Nakuru, ambapo kuna hofu kuwa wanafunzi kadhaa wamepoteza maisha.
Taarifa zinasema moto huo ulianza majira ya saa saba usiku (1:00 usiku) na kuripotiwa takriban saa tisa na nusu usiku (3:30 usiku) Alhamisi, kwa mujibu wa Msalaba Mwekundu Kenya.
Katika taarifa yake, shirika hilo limesema:
“Baada ya tukio la moto lililoripotiwa saa 3:30 usiku katika Chuo cha Wasichana Utumishi, Kaunti ya Nakuru, Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya umefika kusaidia katika operesheni ya dharura inayoendelea.”
Limeongeza kuwa:
“Wahudumu wetu wa kwanza, kikosi cha ambulensi cha EMS Kenya pamoja na wataalamu wetu wa usaidizi wa kisaikolojia wako eneo la tukio kuwasaidia wanafunzi walioathirika pamoja na wahudumu wengine na mamlaka husika.”
Shughuli za uokoaji na tathmini ya tukio hilo bado zinaendelea huku mamlaka zikichunguza chanzo cha moto huo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Bonde la Ufa, Samuel Ndanyi, amesema kuna wanafunzi wasiopungua kumi ambao bado hawajulikani walipo.
“Timu zetu zipo eneo la tukio kukusanya taarifa zaidi na kuwabaini wanafunzi wote kama sehemu ya uchunguzi wa tukio hili. Tuna vifo na ni muhimu familia ziarifiwe kwanza,” alisema.
Wazazi wamefurika katika lango la shule baada ya taarifa za tukio hilo kusambaa Gilgil na maeneo jirani, huku polisi wakizuia idadi kubwa kuingia ndani ya shule na kuruhusu wazazi pekee wakati shughuli za uokoaji zikiendelea.
Wanafunzi waliojeruhiwa wamekimbizwa katika Hospitali ya St. Joseph’s Gilgil kwa matibabu na uchunguzi zaidi.