Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran kuendelea usiku kucha

Mazungumzo ya Marekani na Iran kuhusu kufikia makubaliano ya mwisho ya kusitisha vita yanatarajiwa kuendelea hadi usiku wa manane nchini Uswisi, afisa mwandamizi wa diplomasia wa Marekani anayehusika katika mazungumzo hayo amesema.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Starmer anatafakari mustakabali wake wa kisiasa huku shinikizo la kumtaka ajiuzulu likiongezeka

    Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, anaripotiwa kutafakari mustakabali wake wa kisiasa wakati kukiwa na shinikizo la kutaka atangaze kujiuzulu.

    Hali hiyo imekuja baada ya mshirika wake wa karibu katika Baraza la Mawaziri, Peter Kyle, kusema kuwa Waziri Mkuu alikuwa akizingatia "uhalisia wa kisiasa" kufuatia ushindi wa Andy Burnham katika uchaguzi mdogo wa Makerfield wiki iliyopita, ambao umefungua njia kwake kuwania uongozi wa Chama cha Labour.

    Baada ya matokeo hayo, Starmer amekabiliwa na wito mpya kutoka kwa baadhi ya mawaziri waandamizi wakimtaka kuweka wazi ratiba ya kuondoka kwake madarakani ili kumpisha Burnham.

    Katika pigo jingine kwa kiongozi huyo wa Labour, Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema kuwa Starmer "atajiuzulu kama Waziri Mkuu", huku akikosoa utendaji wake akiwa madarakani.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema Starmer "ameshindwa vibaya" katika sera za uhamiaji na nishati, na akasisitiza tena wito wake wa kufunguliwa zaidi kwa uchimbaji wa mafuta katika Bahari ya Kaskazini.

    Trump aliongeza:

    "Namtakia kila la heri!"

    Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza iliiambia BBC kwamba viongozi hao wawili, ambao walikutana mara ya mwisho katika mkutano wa viongozi wa G7 nchini Ufaransa wiki iliyopita, hawakuwa wamezungumza mwishoni mwa wiki.

    Mara baada ya ushindi wa Burnham, Starmer aliendelea kusisitiza kwamba angepambana na jaribio lolote rasmi la kuondolewa kwenye uongozi wa chama.

    Hii ina maana kuwa kama kutakuwa na changamoto ya uongozi, uchaguzi wa ndani wa Labour utahitajika, ambapo wanachama wa chama pamoja na wafuasi wa vyama vya wafanyakazi vinavyoshirikiana na Labour wataamua mustakabali wa chama hicho.

    Unaweza kusoma;

  2. Kiongozi wa Hezbollah: Haiwezekani kwa majeshi ya Israel kuendelea kubaki nchini Lebanon

    Kiongozi wa Hezbollah, Naim Qassem, alijibu kauli za Waziri Mkuu wa Israel siku ya Jumapili kuhusu majeshi ya Israel kuendelea kubaki katika eneo la usalama kusini mwa Lebanon, akisema:

    "Haiwezekani kwa majeshi ya Israel kubaki nchini Lebanon."

    Aliongeza:

    "Hakuna eneo la usalama kwa Israel. Tuna jeshi la taifa ambalo lina jukumu la kulinda nchi, na sisi tunashirikiana nalo."

    Kiongozi huyo wa Hezbollah alisema katika hotuba iliyorushwa moja kwa moja kwenye televisheni kwamba Israel ni "nchi adui" na kwamba "lazima iondoke nchini Lebanon."

    Pia alilaumu Marekani kwa kuendelea kuwepo kwa majeshi ya Israel nchini Lebanon, akisema kuwa Marekani inabeba jukumu la hali hiyo kuendelea.

    Unaweza kusoma;

  3. Duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran inatarajiwa kuendelea usiku kucha

    Mazungumzo kati ya Marekani na Iran ya kufikia makubaliano ya mwisho ya kumaliza vita yanatarajiwa kuendelea usiku kucha nchini Uswisi, afisa mwandamizi wa Marekani anayeshiriki katika mazungumzo hayo amesema.

    Mazungumzo hayo yalianza Jumapili, kufuatia makubaliano ya wiki iliyopita ya kufikia suluhu ndani ya siku 60.

    Jumapili usiku, mwanadiplomasia huyo wa Marekani alisema kwamba majadiliano yalikuwa yakijikita katika kufafanua baadhi ya ujumbe zilizokuwa hazieleweki kutoka Iran kuhusu kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, utekelezaji wa usitishaji mapigano kusini mwa Lebanon, pamoja na baadhi ya vipengele vya makubaliano ya nyuklia.

    Mapema, Rais wa Marekani, Donald Trump, alikuwa ametishia kuishambulia Iran ikiwa haitaisimamisha Hezbollah huku mapigano kati ya kundi hilo na Israel yakiendelea nchini Lebanon. Iran ilipuuzilia mbali onyo hilo, ikisema iko tayari kupigana.

    Afisa huyo alisema ujumbe wa pande zote mbili, ambao unakutana katika mji wa Lucerne nchini Switzerland, utatumia matokeo ya mazungumzo ya leo kama msingi wa mazungumzo ya kiufundi yatakayoendelea.

    Makubaliano ya awali ya wiki iliyopita yanajumuisha ahadi ya kufikia makubaliano ya mwisho ndani ya siku 60, pamoja na kusitishwa kwa mapigano katika maeneo yote ya mzozo, ikiwemo Lebanon, na kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Hata hivyo, tangu wakati huo kumeshuhudiwa kuongezeka kwa mapigano kati ya Hezbollah na majeshi ya Israel kusini mwa Lebanon, pamoja na mashambulizi ya anga ya Israel ambayo wizara ya afya ya Lebanon imesema yamesababisha vifo vya raia kadhaa, wakiwemo wanawake na watoto.

    Kuongezeka huko kwa mzozo kuliipelekea Marekani kutangaza usitishaji mpya wa mapigano kati ya Israel na Hezbollah siku ya Ijumaa.

    Lakini mapigano na mashambulizi ya anga yaliyoendelea yaliifanya Iran kutangaza Jumamosi kwamba imeufunga Mlango-Bahari wa Hormuz, ingawa takwimu za ufuatiliaji wa meli zinaonesha kuwa vyombo vya majini vimeendelea kupita katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.

    Unaweza kusoma;

  4. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu hii leo.