Starmer anatafakari mustakabali wake wa kisiasa huku shinikizo la kumtaka ajiuzulu likiongezeka

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, anaripotiwa kutafakari mustakabali wake wa kisiasa wakati kukiwa na shinikizo la kutaka atangaze kujiuzulu.
Hali hiyo imekuja baada ya mshirika wake wa karibu katika Baraza la Mawaziri, Peter Kyle, kusema kuwa Waziri Mkuu alikuwa akizingatia "uhalisia wa kisiasa" kufuatia ushindi wa Andy Burnham katika uchaguzi mdogo wa Makerfield wiki iliyopita, ambao umefungua njia kwake kuwania uongozi wa Chama cha Labour.
Baada ya matokeo hayo, Starmer amekabiliwa na wito mpya kutoka kwa baadhi ya mawaziri waandamizi wakimtaka kuweka wazi ratiba ya kuondoka kwake madarakani ili kumpisha Burnham.
Katika pigo jingine kwa kiongozi huyo wa Labour, Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema kuwa Starmer "atajiuzulu kama Waziri Mkuu", huku akikosoa utendaji wake akiwa madarakani.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema Starmer "ameshindwa vibaya" katika sera za uhamiaji na nishati, na akasisitiza tena wito wake wa kufunguliwa zaidi kwa uchimbaji wa mafuta katika Bahari ya Kaskazini.
Trump aliongeza:
"Namtakia kila la heri!"
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza iliiambia BBC kwamba viongozi hao wawili, ambao walikutana mara ya mwisho katika mkutano wa viongozi wa G7 nchini Ufaransa wiki iliyopita, hawakuwa wamezungumza mwishoni mwa wiki.
Mara baada ya ushindi wa Burnham, Starmer aliendelea kusisitiza kwamba angepambana na jaribio lolote rasmi la kuondolewa kwenye uongozi wa chama.
Hii ina maana kuwa kama kutakuwa na changamoto ya uongozi, uchaguzi wa ndani wa Labour utahitajika, ambapo wanachama wa chama pamoja na wafuasi wa vyama vya wafanyakazi vinavyoshirikiana na Labour wataamua mustakabali wa chama hicho.
Unaweza kusoma;
















