Maelfu ya watu wamiminika katika kijiji cha West Pokot kufuatia ripoti ya ugunduzi wa dhahabu
Ripoti kuhusu ugunduzi wa dhahabu katika kijiji cha Cheparor, eneo bunge la Kapenguria kaunti ya West Pokot, nchini Kenya imesababisha wimbi kubwa la watu wanaotafuta utajiri kumiminika katika eneo hilo.
Video zilizotazamwa zilionyesha umati mkubwa wa watu ukiwa ametapakaa katika eneo la wazi, wakichimba kwa kutumia zana duni huku wengine wakikusanya udongo kwenye mabakuli na magunia kabla ya kuondoka nao.
Picha hizo zilionyesha wanaume na wanawake wakifanya kazi pamoja; baadhi wakichimba mashimo madogo huku wengine wakipanga foleni kuchukua udongo uliochimbwa, wakionekana kuwa na nia ya kuuchunguza zaidi mahali pengine ili kuona kama una chembechembe za madini hayo ya thamani.
Kulingana na taarifa zinazosambaa mtandaoni, harakati hizo zilianza baada ya wavulana wawili kudaiwa kugundua kitu kilichoaminika kuwa dhahabu katika eneo hilo.
Hata hivyo, bado haijafahamika wazi iwapo ugunduzi huo ulikuwa wa kitu kimoja tu au iwapo eneo hilo lina akiba ya dhahabu inayoweza kuchimbwa kibiashara.
Mamlaka husika hazikuwa zimethibitisha ripoti hizo.
Video hiyo pia ilionyesha watu wakifika kutoka pande mbalimbali, huku baadhi ya ripoti zikidai kuwa watu wanaotafuta utajiri walisafiri kutoka nchi jirani ya Uganda na sehemu nyingine za Kenya baada ya habari za ugunduzi huo kusambaa.