Utafiti waonesha mafanikio makubwa ya chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi
Takriban maisha ya watu 200 yameokolewa nchini Uingereza kufikia sasa kutokana na chanjo inayokinga saratani ya shingo ya kizazi, hii ikiwa ni kulingana na uchambuzi uliochapishwa katika jarida la la Lancet.
Utafiti huo wa kwanza wa aina yake umeonyesha kwamba vifo vimepungua sana tangu wasichana wenye umri wa kwenda shule walipopewa chanjo ya human papillomavirus (HPV) mwaka 2008.
Ripoti ya utafiti huo inaonesha kuwa kati ya 2020 na 2024, hakuna vifo vya saratani ya shingo ya kizazi vilirekodiwa kwa wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 24 - mara ya kwanza kutokea kwa kipindi cha miaka mitano.
Bila chanjo, takribani vifo ishirini na vitatu vingetarajiwa.
Prof Peter Sasieni, mtafiti mkuu katika Chuo Kikuu cha Queen Mary cha London amesema:
"Inashangaza kufikiria kwamba chanjo inaweza kukaribia kumaliza aina fulani ya saratani,"
Utafiti huo pia uligundua kuwa watoto hao waliochanjwa wakiwa na umri wa miaka 12 au 13 sasa hawakabiliwi kabisa na hatari ya kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo kabla ya umri wa miaka 30.
Kabla ya kampeni ya chanjo ya HPV, takribani vifo 20 kila mwaka vilikuwa vikirekodiwa katika kundi hilo la umri.
Kwa ujumla, saratani ya shingo ya kizazi bado ni saratani ya 14 kati ya wanawake nchini Uingereza, na watu 3,300 hugunduliwa kila mwaka.
Inafikiriwa kuwa HPV, virusi ambavyo huenezwa kwa mgusano wa karibu wa ngozi kwa ngozi, husababisha asilimia 99 ya maaambukizi yote ya saratani hiyo.
Maambukizi mengi ya HPV hupita bila matatizo yoyote, lakini mengine husababisha mabadiliko yasiyo ya kawaida ya seli na yanaweza kusababisha saratani miaka mingi baadaye.
Soma zaidi: