Moja kwa moja, Iran yasema makubaliano ya kusitisha mapigano na Marekani yamevunjika

Tehran yasema mashambulizi mapya ya Marekani yamefuta msingi wa maelewano kati ya pande hizo mbili.

Muhtasari

Iran yasema makubaliano na Marekani yamevunjika

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Hispania yafuzu fainali baada ya kuichapa Ufaransa

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Beki wa Hispania na mchezaji bora wa mechi, Pedro Porro, amesema kufuzu kwa timu yake ni ndoto aliyokuwa akiisubiri kwa muda mrefu.

    "Hii ni ndoto iliyotimia kwangu. Ilikuwa ndoto yangu kubwa zaidi. Nina furaha sana kwa timu. Tulicheza vizuri kuanzia mwanzo hadi mwisho na leo tulifanya kila tulichoweza ili kufuzu," alisema Porro.

    Akizungumzia ushindi dhidi ya Ufaransa, Porro alisema walijua wangekutana na mpinzani mgumu lakini walitekeleza mpango wao ipasavyo.

    "Tulijua tunakutana na timu ngumu sana. Huu ni ushindi wa timu nzima, si wangu pekee. Nawapongeza wachezaji wote kwa kiwango walichoonyesha."

    Kuhusu jinsi walivyowadhibiti Wafaransa, Porro alisema umiliki wa mpira ulikuwa sehemu muhimu ya mkakati wao.

    "Tulijua kumiliki mpira kungetusogeza karibu na ushindi. Mashambulizi yao ya kushtukiza ndiyo silaha yao kubwa, na kuyazuia ilikuwa jambo muhimu."

    Porro pia alisema alitolewa uwanjani baada ya kuhisi hangeweza kuendelea kuchangia zaidi, akisisitiza kuwa ushindi huo ulitokana na mchango wa kikosi kizima.

    "Nilihisi siwezi kuchangia zaidi. Ushindi huu umeletwa na wachezaji wote 26. Sasa tunaelekeza nguvu zetu kwenye fainali."

    Alimalizia kwa kusema kuwa licha ya uchovu, Hispania itajipanga upya na kupambana kwa nguvu zote katika mchezo wa fainali.

    Soma Zaidi:

  2. Maseneta wa Democratic wazuia muswada wa ulinzi wa Marekani kupinga vita na Iran

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maseneta wa Chama cha Democratic nchini Marekani wamekwamisha kupitishwa kwa Muswada wa Mwaka wa Sera ya Ulinzi, wakionyesha kupinga kuendelea kwa vita dhidi ya Iran.

    Muswada huo, unaojulikana kama National Defense Authorization Act (NDAA), umeshindwa kusonga mbele baada ya kuungwa mkono na maseneta 50 huku 46 wakipinga.

    Ingawa bado unahitaji hatua nyingine kabla ya kuwa sheria, matokeo hayo yanaonyesha mgawanyiko mkubwa katika Seneti kuhusu sera ya Marekani dhidi ya Iran na athari zake kwa bajeti ya Wizara ya Ulinzi.

    Seneta Richard Blumenthal, mwanachama wa chama cha Democratic na kiongozi wa upinzani katika Kamati ya Seneti ya Huduma za Kijeshi, alisema muswada huo kwa sasa unaendeleza ufadhili wa vita dhidi ya Iran.

    "Kwa mtazamo wangu, sheria hii inaendeleza ufadhili wa vita, huku utawala wa sasa ukikosa uwajibikaji," alisema.

    Blumenthal alisema hataunga mkono muswada huo hadi utawala wa Rais Donald Trump utoe mkakati wazi kuhusu Iran na upate idhini ya Bunge kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Vita.

    Naye Seneta Tammy Duckworth alisema asingepigia kura muswada huo kusonga mbele isipokuwa marekebisho aliyopendekeza yapitishwe, yakilenga kuzuia fedha zaidi kutumika kufadhili operesheni za kijeshi za kushambulia Iran.

    Soma Zaidi Hapa:

  3. Trump afuta pendekezo la tozo ya asilimia 20 kwa meli zinazopita Hormuz

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump ameondoa pendekezo lake la kutoza ada ya asilimia 20 kwa mizigo yote inayopitia Mlango wa Bahari wa Hormuz, akisema badala yake atategemea mikataba mikubwa ya biashara na uwekezaji kutoka mataifa ya Ghuba.

    Hatua hiyo imekuja saa chache kabla ya Jeshi la Marekani kupitia Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) kurejesha kizuizi dhidi ya bandari za Iran na kuanzisha duru mpya ya mashambulizi dhidi ya malengo ya Iran.

    CENTCOM ilisema mashambulizi hayo yanalenga kudhoofisha uwezo wa Iran wa kushambulia meli za kibiashara zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Mashambulizi hayo yanafuatia mapigano mapya kati ya Marekani na Iran, ambayo yamesababisha bei ya mafuta kupanda huku shughuli za usafirishaji wa mafuta kupitia Hormuz zikipungua kwa kiasi kikubwa.

    Iran ilisema imelenga vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Bahrain na Jordan, baada ya awali kushambulia meli mbili za Umoja wa Falme za Kiarabu.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema:

    "Nimeamua kuondoa tozo ya asilimia 20 ya Marekani na badala yake mataifa ya Ghuba yatawekeza na kufanya mikataba mikubwa ya biashara nchini Marekani."

    Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu mpango huo.

    Trump pia alisema Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kuwa wazi kwa meli zote isipokuwa zile zinazofanya biashara na Iran.

    Baadaye, akizungumza mjini Washington, Trump alisema hakupendelea wazo la kutoza ada kwa meli zinazopita Hormuz, lakini akaongeza kuwa si haki kwa Marekani kubeba jukumu la kulinda njia hiyo muhimu ya baharini kwa manufaa ya dunia nzima.

    Kwa upande wake, Iran imesema itaendelea kusimamia Mlango wa Bahari wa Hormuz licha ya hatua za Marekani.

    Unaweza kusoma;

  4. Iran yasema makubaliano ya kusitisha mapigano na Marekani yamevunjika

    D

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa masuala ya kisheria Iran Kazem Gharibabadi amesema hakuna tena kinachoitwa Makubaliano ya Islamabad kati ya Tehran na Washington, akidai kuwa mashambulizi mapya ya Marekani yameharibu kabisa msingi wa maelewano yaliyokuwapo.

    Kauli hiyo imekuja baada ya Marekani kuanzisha mashambulizi mapya katika pwani ya kusini mwa Iran na Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) kutangaza kurejesha kizuizi cha majini dhidi ya bandari za Iran.

    "Hakuna tena kinachoitwa Makubaliano ya Islamabad. Msingi wa maelewano kati ya Iran na Marekani umeharibiwa kabisa," alisema Naibu Waziri huyo.

    Mapema Jumatano, milipuko kadhaa iliripotiwa katika maeneo ya kusini mwa Iran kufuatia mashambulizi ya Marekani.

    Kwa kujibu mashambulizi hayo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na jeshi la Iran yalisema yamelenga vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Kuwait, Bahrain na Jordan kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani.

    Mvutano kati ya Iran na Marekani umeendelea kuongezeka huku pande zote zikiendeleza mashambulizi na hatua za kijeshi katika eneo la Ghuba.

    Soma Zaidi:

  5. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.