Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Axio: Iran, Oman na Marekani zakaribia kufikia makubaliano ya kufungua tena Mlango-bahari wa Hormuz

Axios iliripoti, ikinukuu vyanzo viwili vya kikanda na afisa wa Marekani, kwamba Marekani, Iran, na Oman ziko karibu kufikia makubaliano ya muda ya kufungua tena Mlango-bahari wa Hormuz

Muhtasari

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu

  1. Infantino aitisha kikao cha FIFA huku ukosoaji ukiongezeka

    Gianni Infantino amewaita viongozi wakuu wa shirikisho la soka duniani (FIFA) kwenye mkutano nchini Morocco siku ya Jumatano, kufuatia siku nyingine ambapo rais wa shirikisho hilo amekabiliwa na ukosoaji mkali kuhusu mpango wake uliositishwa wa kuuza kuuza hisa za mashindano ya FIFA kwa wawekezaji binafsi.

    Mkuu wa maendeleo ya soka duniani wa FIFA, Arsene Wenger, Katibu Mkuu Mattias Grafstrom, na Mwana mfalme Ali, rais wa Shirikisho la Soka la Jordan, wote walionyesha wazi kupinga mpango wa Infantino unaojulikana kama 'Fifa Forward Enterprise'.

    Infantino, ambaye amekuwa nchini Morocco kwa wiki iliyopita, aliitisha mkutano wa maafisa watendaji mjini Rabat katika juhudi za kutafuta suluhisho la utata huo.

    Katika taarifa iliyotolewa kupitia FIFA, Wenger alisema kuwa kusitisha mpango huo kulikuwa "jambo la lazima kabisa na lisilo na shaka yoyote".

    Grafstrom alielezea wiki iliyopita kama "mfululizo wa matukio ya kusikitisha na ya kulaumiwa" katika barua pepe ya ndani iliyotumwa kwa wafanyakazi wa FIFA.

    Wakati huo huo, Mwana mfalme Ali aliishutumu FIFA kwa kuunda hali ambayo "inaweza kuchukuliwa kama shinikizo la kulazimisha mambo" kuhusiana na fedha za zawadi ambazo hazijalipwa na uungaji mkono kwa ajili ya kuchaguliwa tena kwa Infantino.

    Tangu mwaka 2019, Wenger amekuwa akishikilia wadhifa unaohusisha uchambuzi wa takwimu za mchezo huo, mafunzo ya mtandaoni ya FIFA, na mashindano ya vijana.

    Aliyekuwa kocha mkuu wa Arsenal hapo awali aliunga mkono pendekezo la Infantino la kuandaa Kombe la Dunia la wanaume kila baada ya miaka miwili

  2. Asilimia 87 ya wafanyakazi wa Kenya waripoti msongo wa mawazo - Utafiti

    Sekta ya biashara nchini Kenya inakabiliwa na mgogoro unaoongezeka wa ustawi kazini, huku utafiti mpya ukionyesha kuwa takriban wafanyakazi tisa kati ya kumi (87%) wanaripoti kupata msongo wa mawazo, na kuibua wasiwasi mpya kuhusu tija, ushiriki wa wafanyakazi na utendaji.

    Matokeo hayo, yaliyotolewa na shirika la Niche Human Capital Advisory, yanajiri wakati ambapo waajiri wanakabiliwa na kuongezeka kwa uchovu, mabadiliko ya matarajio ya wafanyakazi na kuongezeka kwa ushindani wa vipaji.

    Nchini humo, asilimia 80.4% ya wafanyakazi wanaripoti msongo wa mawazo wa wastani hadi uliokithiri kazini, huku 67.8% ya wafanyakazi katika Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara wakiripoti uchovu wa kihisia na uchovu, wakisisitiza ukubwa wa changamoto inayowakabili waajiri.

    Wakati huo huo, 82.5% ya wafanyakazi wanaamini mashirika yanahitaji kufanya zaidi ili kusaidia kuimarisha afya ya akili.

  3. Axio: Iran, Oman na Marekani zakaribia kufikia makubaliano ya kufungua tena Mlango-bahari wa Hormuz

    Axios iliripoti, ikinukuu vyanzo viwili vya kikanda na afisa wa Marekani, kwamba Marekani, Iran, na Oman ziko karibu kufikia makubaliano ya muda ya kufungua tena Mlango-bahari wa Hormuz.

    Kulingana na vyanzo vya habari vya Axios, serikali ya Marekani inatarajia kutangaza makubaliano hayo siku ya Jumatano.

    Maelezo ya makubaliano hayo yanayoweza kufikiwa bado hayajatolewa na hakuna hata upande mmoja kati ya pande hizo tatu uliothibitisha rasmi ripoti hiyo; hata hivyo, siku ya Jumanne, vyombo vya habari vya Marekani vikinukuu vyanzo vyao vilijaribu kuripoti vipengele vikuu vya mazungumzo hayo na masharti yanayotakiwa na pande husika. Kama ilivyoripotiwa na Axios, vipengele vya mazungumzo hayo vilikuwa kama ifuatavyo:

    • Meli zote zinazoingia Ghuba ya Uajemi zitasafiri kupitia njia ya kaskazini na kupita katika maji ya Iran.
    • Meli zote zinazotoka Ghuba ya Uajemi kuelekea Bahari ya Oman zitapita kupitia njia ya kusini na katika maji ya Oman, kwa uratibu na Iran.
    • Katika kipindi cha utekelezaji wa siku 60 cha makubaliano hayo ya muda, hakuna ushuru au ada yoyote itakayotozwa kwa meli zinazopita.
    • Pande zinazohusika na makubaliano hayo zitajitolea kutekeleza operesheni ya kuondoa mabomu ya baharini katika njia ya katikati ya Mlango-bahari wa Hormuz ndani ya siku 30.
    • Mara tu njia ya katikati itakapokuwa imesafishwa, itatumika kwa ajili ya usafiri wa meli zinazoingia na kutoka. Utaratibu wa matumizi ya njia hiyo utaamuliwa katika makubaliano ya kudumu yatakayojadiliwa kati ya Iran na Oman.
  4. Vifo vya ajabu vya tembo nchini Kenya vyaibua maswali kuhusu dawa za kuuwa wadudu

    Habari kwamba vifo vya hivi karibuni vya tembo 15 huenda vilisababishwa na dawa za kuuwa wadudu zilizopulizwa kwenye mashamba ya nyanya yanayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Amboseli vimezua wasiwasi na maswali nchini Kenya.

    Wiki iliyopita, Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini Kenya (KWS) lilisema kuwa baadhi ya tembo hao waliokufa kati ya tarehe 24 Juni na 24 Julai walionyesha dalili za "kupooza kwa sehemu ya mwili," jambo lililoashiria sumu inayotokana na kemikali ya 'cyanide' inayopatikana katika dawa hizo za kuuwa wadudu.

    Hata hivyo, wanaharakati wa uhifadhi wameiambia BBC kwamba huenda hiyo isiwe ndiyo picha kamili ya hali halisi.

    Wakulima tuliozungumza nao katika eneo hilo pia walionyesha kutokuwa na uhakika na madai hayo.

    "Tumeishi na wanyamapori hawa kwa miongo kadhaa na hatujawahi kushuhudia jambo kama hili," Daniel Nina, anayewakilisha baadhi ya wamiliki wa ardhi katika eneo hilo, aliambia BBC.

    "Ndiyo maana tunajiuliza ni kwa nini jambo hili linatokea leo."

    Mashamba hayo ya nyanya yanapatikana katika eneo la Kimana, ambalo ni sehemu ya njia ya wanyama inayounganisha Hifadhi ya Taifa ya Amboseli na Hifadhi ya Taifa ya Tsavo kusini mwa Kenya.

    Eneo hilo kubwa, linalojulikana kama mfumo wa ikolojia wa Amboseli, linapakana na nchi jirani ya Tanzania na ni njia inayotumiwa na zaidi ya tembo 2,000 kutafuta chakula na maji.

    Mashamba hayo hustawi kutokana na maji yanayotiririka kutoka Mlima Kilimanjaro ulio karibu, na hutoa mazao yanayouzwa katika masoko ya Nairobi, mji mkuu wa Kenya, na maeneo mengine.

    Daktari Mkuu wa Mifugo katika Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini Kenya, Dkt. Isaac Lekolool, alituambia kuwa waligundua chembechembe za sumu ya 'cyanide' katika sampuli zilizochukuliwa kutoka kwenye matumbo ya tembo hao.

    Anasema kuwa hawajaacha uwezekano wa sumu kuwekwa makusudi, lakini kwa sasa haiwezekani kubaini nini hasa kilichosababisha vifo vya tembo hao.

    "Ni vigumu kusema kwa sababu hatujawahi kushuhudia visa vya aina hii hapo awali. Ni tukio la kipekee, na lilitokea ndani ya kipindi cha takriban mwezi mmoja," alisema Lekolool.

    Dhana yao ya awali ni kwamba tembo hao walikumbana na sumu hiyo kupitia dawa za kuuwa wadudu zilizopulizwa katika mashamba ya nyanya yaliyo karibu.

    "Huenda ilitokea bila kukusudiwa. Labda watu walikuwa wakijaribu kudhibiti wadudu kwenye mazao yao, na hilo linaweza kuwa ndilo chanzo."

    Tatizo la dawa za kuua wadudu.

    Ripoti ya mwaka 2024 kutoka kwa shirika la Kenya linaloshughulikia usalama wa chakula, Route to Food, ilibaini mkulima mmoja katika eneo la Kimana akitumia dawa ya kuuwa wadudu iliyokuwa na "kiambato amilifu" ambacho ni " kemikali ya sianidi".

    Wangunyu Njuguna, mwandishi wa ripoti hiyo, alisema kuwa licha ya kupigwa marufuku nchini Kenya, baadhi ya kemikali hatari za kilimo huingizwa nchini kwa njia ya magendo kupitia mpaka wa Tanzania.

    "Tatizo kubwa ni kwamba hatutekelezi viwango sawa katika eneo hili," alisema Njuguna. "Hakuna anayekagua ninachoenda kununua ninapovuka mpaka, hivyo naweza kwenda kununua chochote na kupita mpakani bila mtu yeyote kunizuia."

    Kemikali hatari sana zinapatikana kwa wingi katika mashamba ya Kenya na baadhi yake zimehusishwa na magonjwa hatari.

    Ingawa kuna kanuni zinazopiga marufuku kemikali haramu za kilimo, utekelezaji wake ni dhaifu na hakuna umakini wa kutosha kuhusu jinsi kemikali hizo zinavyoweza kuathiri wanyama.

  5. Tazama Video ya droni ya Urusi ikimfukuza mchuuzi nchini Ukraine

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amechapisha video kwenye mitandao ya kijamii inayoonyesha droni ikimwinda mwanamume kusini mwa Ukraine, akisema kuwa tukio hilo linaonyesha shambulio la Kirusi la aina ya "safari" (uwindaji wa burudani) dhidi ya raia.

    Video hiyo inaonyesha droni ikimfuatilia mchuuzi katika barabara ya jiji katika eneo la Kherson.

    Mwanamume huyo anajaribu kujiepusha na droni inayoning'inia juu yake, kabla ya droni hiyo kuanza kumkimbiza huku akikimbia kuzunguka gari jeupe la aina ya van.

    Hatimaye, droni hiyo inashuka kwa kasi na kulipuka ilipomgonga.

    Mwanamume huyo alinusurika akiwa na majeraha mengi ya vipande vya chuma, mtikiso wa ubongo na mshtuko wa kisaikolojia, daktari alisema.

    Matumizi ya droni zinazoendeshwa kwa mbali dhidi ya raia, jambo ambalo wakati mwingine huitwa "uwindaji wa binadamu" (human safari) yamekuwa yakitumiwa mara kwa mara na Warusi kuwatia hofu wakazi wa maeneo ya mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine.

    "Lazima dunia ione hili," Zelensky aliandika kwenye Telegram. "Lazima ione kila ushahidi kwamba Urusi imepoteza akili, na kila ukweli kwamba askari wa Urusi wanafurahia kuua na kuwatesa watu."

    Video hiyo ilionyesha "uhalifu wa kivita wa kikatili," alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha.

    Vitendo hivyo vya uwindaji vilikuwa "mkakati wa makusudi na wa kimfumo wa Urusi," Sybiha alisema.

    "Mtu huyo mwenye tabia ya kikatili na ya kufurahia mateso anayeendesha droni hii anajua kwamba anamshambulia raia."

    Aliongeza kuwa shambulio hilo lilikuwa sehemu ya kampeni ya makusudi ya Urusi ya kuwatisha raia na akataka kulaaniwa kimataifa.

  6. Klabu ya Uturuki Trabzonspor yaanza mazungumzo ya kumsajili Mohamed Salah

    Klabu ya Trabzonspor ya Uturuki imetangaza kuwa imeanza mazungumzo ya kumsajili Mohamed Salah.

    Mshambuliaji huyo raia wa Misri, mwenye umri wa miaka 34, aliondoka Liverpool mwishoni mwa msimu uliopita na kwa sasa yuko katika mazungumzo ya kujiunga na timu hiyo kama mchezaji huru, bila kufungwa na mkataba rasmi na klabu yoyote ya michezo.

    Katika taarifa yake, Trabzonspor imesema kuwa Salah atawasili Istanbul siku ya Jumatano.

    Taarifa hiyo iliongeza: "Mchezaji huyo anatarajiwa kuwasili Trabzon jioni hiyo hiyo."

    Iliongeza pia: "Tarehe ya kuwasili kwa mchezaji huyo na maelezo mengine kuhusu ratiba ya mapokezi yake huko Trabzon yatatangazwa kupitia njia rasmi za mawasiliano za klabu hiyo katika kipindi cha siku hiyo."

  7. Bei ya mafuta yashuka kufuatia matumaini ya kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz

    Bei ya mafuta ilishuka hadi kiwango cha chini cha wiki tatu Jumanne huku maafisa wakuu wa Marekani wakiongeza matumaini ya makubaliano na Iran ya kufungua tena njia kuu ya maji ya Hormuz.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Waziri wa Hazina Scott Bessent wote walitangaza kwamba mazungumzo yameendelea ili kuruhusu uwezekano wa usafirishaji kuanza tena haraka iwezekanavyo wiki hii.

    Gharama ya pipa la mafuta ghafi ya Brent, kipimo cha kimataifa cha bei ya mafuta, ilishuka kwa karibu 5% hadi chini ya $80 (£60) kutokana na habari za usumbufu wa usambazaji unaoweza kupungua.

    Lakini kushindwa kwa mazungumzo ya awali katika miezi ya hivi karibuni ili kupunguza mzozo kati ya Marekani na Iran kumesababisha soko la mafuta tete, huku madereva hatimaye wakiathiriwa na bei kubwa za mafuta kwenye pampu.

    Siku ya Jumanne, pamoja na kushuka kwa mafuta ghafi ya Brent, bei za kati za Marekani Magharibi mwa Texas zilishuka kwa zaidi ya 5%, hadi $76 kwa pipa.

    Mikataba yote miwili ilishuka hadi viwango vyao vya chini kabisa tangu Julai 13.

    Rubio alisema kumekuwa na maendeleo yaliyopatikana katika majadiliano kuhusu kupeleka meli zaidi kupitia njia hiyo na Iran na Oman.

    "Kumepatikana maendeleo katika mazungumzo hayo, lakini bado hayajakamilika. Tunatumai hilo litatokea hivi karibuni," aliwaambia waandishi wa habari katika Wizara ya Mambo ya Nje.

    Bessent alisema makubaliano ya kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz yanaweza kuafikiwa siku ya Jumanne au Jumatano.

  8. Meli ya India yazama baada ya kupigwa kombora karibu na maji ya Yemen

    Waziri wa Usafirishaji wa India anasema meli ya India ilipigwa na kitu kilichorushwa, na kusababisha ipinduke na kuzama karibu na maji ya Yemen.

    Alisema: "Wanamaji wote 14 waliokuwa kwenye meli hiyo waliokolewa salama na Kikosi cha Walinzi wa Pwani cha Yemen."

    Wizara ya Mambo ya Nje ya India ililaani shambulio hilo "vikali" katika taarifa yake.

    "Tunalaani shambulio dhidi ya meli ya kibiashara yenye bendera ya India, MSV Faiz Noor Alia, ambayo ilizama katika Bahari ya Shamu karibu na pwani ya Yemen mnamo Agosti 4, 2026. Raia wote 13 wa India wameokolewa," wizara hiyo ilisema katika taarifa..

  9. Bloomberg: Iran inazingatia kuruhusu Ulaya kushiriki katika kuondoa mabomu ya baharini yaliotegwa katika Mlango-bahari wa Hormuz

    Shirika la habari la Bloomberg liliripoti, likinukuu wanadiplomasia wenye taarifa za ndani, kwamba Iran inafikiria kuonyesha utayari kwa nchi za Ulaya kushiriki katika shughuli za kuondoa mabomu yaliotegwa baharini katika Mlango-bahari wa Hormuz; hatua ambayo inaweza kuwa sehemu ya makubaliano ya kurejesha hali ya kawaida ya usafirishaji katika njia hiyo ya maji na kurahisisha mazungumzo ya amani na Marekani.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Iran imesisitiza mara kwa mara katika misimamo yake ya hadharani kwamba haitaruhusu nchi za kigeni kushiriki katika shughuli za kuondoa mabomu hayo katika njia hiyo muhimu ya kimkakati kwa usafirishaji wa mafuta na gesi asilia.

    Hata hivyo, kulingana na wanadiplomasia waliozungumza na Bloomberg kwa sharti la kutotajwa majina kutokana na unyeti wa suala hilo, Tehran imelainisha msimamo wake kiasi katika mikutano ya faragha katika wiki za hivi karibuni na inazingatia uwezekano wa nchi za Ulaya kushiriki katika operesheni hiyo.

    Bloomberg iliripoti siku ya Jumanne kwamba iwapo mabadiliko hayo yatatekelezeka, hatua hiyo inaweza kuwa sehemu ya juhudi za kidiplomasia za kurejesha usalama wa usafirishaji katika Mlango-bahari wa Hormuz na kupunguza mivutano kati ya Iran na Marekani

  10. CBS: Marekani imetumia karibu akiba yake yote ya makombora ya masafa marefu katika vita dhidi ya Iran

    Vyanzo viwili vimeiambia CBS News - mshirika wa BBC nchini Marekani - kwamba Marekani imetumia karibu akiba yake yote ya dunia nzima ya makombora ya masafa marefu yenye usahihi wa hali ya juu wakati wa vita dhidi ya Iran.

    Kulingana na ripoti hii, Marekani imetumia karibu makombora yake yote ya aina ya *Army Tactical Missile System* (ATACMS) na makombora ya kushambulia kwa usahihi (*Precision Strike Missiles*) katika Operesheni Epic Fury.

    Awali, Reuters iliripoti kuwa Marekani ilikuwa imetumia "karibu makombora yote" ya masafa marefu yenye usahihi wa hali ya juu katika operesheni hii.

    CBS iliripoti hapo awali kuwa akiba ya Marekani ya makombora ya kuzuia mashambulizi (*interceptor missiles*) na makombora ya masafa marefu imepungua sana, na jambo hili limekuwa changamoto ya ndani kwa serikali.

    Kulingana na ripoti hiyo, Marekani haiwezi kuendelea na mwenendo huu kwa kasi ileile iliyotumika kumaliza akiba ya silaha hizo mwanzoni mwa vita dhidi ya Iran.

    Maafisa wa Marekani wamesema kuwa akiba ya makombora haya ni finyu, lakini suala la dharura zaidi ni idadi ya makombora ya kuzuia mashambulizi ya aina ya Patriot na THAAD, ambayo yanatumika kwa kasi kubwa kuliko uwezo wa viwanda vya ulinzi vya Marekani wa kuyazalisha.

    Sean Parnell, msemaji mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon), alisema katika taarifa kwa CBS:

    "Jeshi la Marekani ndilo jeshi lenye nguvu zaidi duniani na lina kila kitu kinachohitajika kutekeleza majukumu yake wakati wowote na mahali popote ambapo rais ataamua. Tumefanya operesheni kadhaa zilizofanikiwa katika maeneo mbalimbali huku tukihakikisha kuwa jeshi la Marekani lina akiba kubwa ya uwezo wa kulinda watu na maslahi ya taifa."

    Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegsett, hapo awali alitupilia mbali wasiwasi kuhusu kupungua kwa akiba ya silaha za Marekani. Aliambia CBS mnamo Julai 14:

    "Hii ni habari ya kubuni ambayo vyombo vya habari vinataka kuisambaza. Hatimaye, akiba yetu iko katika hali nzuri na inaendelea kuimarika zaidi."

    Ripoti hii inakuja wakati matumizi makubwa ya makombora ya kuzuia mashambulizi na silaha zenye usahihi wa hali ya juu katika vita vya hivi karibuni yamechochea mijadala mjini Washington kuhusu uwezo wa uzalishaji wa viwanda vya ulinzi vya Marekani na utayari wake kwa mzozo wa muda mrefu.

  11. Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja