Moja kwa moja, Iran na Marekani zahitimisha mazungumzo Doha bila dalili za amani ya kudumu

Duru hii ya mazungumzo ya Iran na Marekani ilijikita zaidi katika masuala ambayo pande hizo zilisema yalikuwa tayari yameshughulikiwa chini ya makubaliano ya muda yaliyotangazwa wiki mbili zilizopita.

Muhtasari

Iran na Marekani zahitimisha mazungumzo Doha bila dalili za amani ya kudumu

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Marekani yafikiria kuhamisha wanajeshi wake kutoka Saudi Arabia - Gazeti la Wall Street

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kwa mujibu wa gazeti la Wall Street Journal Marekani inatafakari kupunguza au kuhamisha baadhi ya wanajeshi na vifaa vyake vya kijeshi kutoka Saudi Arabia, hatua inayotokana na mvutano unaoongezeka kati ya Washington na Riyadh kuhusu vita vya Iran na usalama wa usafiri wa baharini katika Mlango wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Saudi Arabia ilikataa kuruhusu matumizi ya baadhi ya kambi zake za kijeshi na anga yake wakati Marekani ilipoanzisha operesheni ya kulinda usafiri wa meli katika Mlango wa Hormuz mapema mwaka huu.

    Hatua hiyo, kwa mujibu wa maafisa wa Marekani waliozungumza na gazeti hilo, iliiweka Washington katika hali ngumu na kuathiri utekelezaji wa operesheni ya kijeshi iliyopewa jina la Project Freedom, ambayo Rais Donald Trump alikuwa ameitangaza kwa lengo la kuhakikisha usalama wa meli zinazopita katika njia hiyo muhimu ya baharini.

    Ripoti hiyo inaongeza kuwa miongoni mwa hatua zinazozingatiwa ni kuhamisha baadhi ya wanajeshi na vifaa vya kijeshi kwenda mataifa kama Israel na Jordan, ambayo Washington inaamini yalishirikiana kwa karibu zaidi wakati wa mzozo na Iran.

    Hata hivyo, Wall Street Journal imesisitiza kuwa hakuna uamuzi wa mwisho uliotolewa kuhusu uwezekano wa kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani kutoka Saudi Arabia, na kwamba kwa sasa suala hilo liko katika hatua ya kutathmini hatua mbalimbali.

    Hadi sasa, maafisa wa Marekani hawajathibitisha wala kukanusha uwezekano wa kuondolewa kwa wanajeshi wao kutoka Saudi Arabia hivi karibuni.

    Unaweza kusoma;

  2. Dakika tatu za maajabu zaiondoa Senegal Kombe la Dunia

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Senegal imeondolewa kwenye Kombe la Dunia 2026 kwa njia ya kusikitisha baada ya kupoteza mabao 3-2 dhidi ya Ubelgiji katika muda wa nyongeza, licha ya kuwa ilikuwa inaongoza kwa mabao mawili hadi dakika za mwisho za mchezo.

    Matokeo hayo yanaifanya Senegal kuwa timu ya tano kutoka Afrika kuaga mashindano hayo, ikiifuata Afrika Kusini, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Tunisia.

    Kwa sasa, Morocco ndiyo timu pekee ya Afrika iliyofuzu hatua ya 16 bora baada ya kuwaondoa Uholanzi kwa mikwaju ya penalti.

    Algeria, Misri, Cape Verde na Ghana bado zinasaka nafasi ya kuungana nao.

    Senegal ilianza vyema mechi hiyo ya hatua ya 32 bora mjini Seattle, ikitangulia kwa bao la Habib Diarra dakika ya 25 kabla ya Ismaila Sarr kuongeza la pili dakika ya 51 na kuifanya ionekane kuwa njiani kutinga hatua inayofuata.

    Hata hivyo, ndani ya dakika tatu za mwisho za muda wa kawaida, Belgium ilibadili kabisa mchezo. Romelu Lukaku, aliyeingia akitokea benchi, alifunga dakika ya 86 kabla ya nahodha Youri Tielemans kusawazisha dakika ya 89 na kuupeleka mchezo katika muda wa nyongeza.

    Senegal ilijitahidi kuhimili shinikizo katika muda wa nyongeza, lakini katika dakika ya 120+5, Tielemans alipata penati na kuifunga mwenyewe, akiipa Ubelgiji ushindi wa mabao 3-2 na tiketi ya hatua ya 16 bora.

    Ubelgiji sasa itakutana na Marekani katika hatua ya 16 bora baada ya Wamarekani kuifunga Bosnia na Herzegovina mabao 2-0.

    Unaweza kusoma;

  3. Iran na Marekani zahitimisha mazungumzo Doha bila dalili za amani ya kudumu

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Iran na Marekani zimehitimisha duru nyingine ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja Jumatano bila kuonyesha dalili za kupiga hatua kuelekea makubaliano ya amani ya kudumu, huku mazungumzo yakijikita zaidi katika masuala ambayo pande hizo zilisema yalikuwa tayari yameshughulikiwa chini ya makubaliano ya muda yaliyotangazwa wiki mbili zilizopita.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imesema hatua chanya zimepatikana katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yaliyofanyika mjini Doha, huku pande hizo zikikubaliana kuendeleza mazungumzo baada ya mazishi ya kiongozi wa zamani wa juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.

    Soma zaidi:

  4. Hujambo natumai umzima, karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.