Moja kwa moja, Nigeria yasema raia wake wawili wameuawa Afrika Kusini huku mashambulizi dhidi ya wahamiaji yakiongezeka

Nigeria imesema kuwa raia wake wawili wameuawa nchini Afrika Kusini "wakati ambapo raia wa kigeni wanaendelea kulengwa isivyo haki" nchini humo.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Vietnam, kitovu cha kimataifa cha bidhaa bandia za kifahari, yaanzisha msako mkali dhidi ya soko la biashara haramu

    Mikoba yenye chapa ya mbunifu maarufu wa Ufaransa, Louis Vuitton, ni miongoni mwa bidhaa zinazopendwa zaidi katika soko la bidhaa bandia.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mikoba yenye chapa ya mbunifu maarufu wa Ufaransa, Louis Vuitton, ni miongoni mwa bidhaa zinazopendwa zaidi katika soko la bidhaa bandia.

    Mapema mwaka huu, polisi wa Vietnam walipovamia maghala mawili yaliyoko nje kidogo ya mji wa Ho Chi Minh, walikuta zaidi ya jozi 23,000 za ndala zilizokuwa na nembo za Nike, Adidas, Crocs na Gucci.

    Hata hivyo, kampuni hizo hazikuwa na uhusiano wowote na maghala hayo. Ndala zote zilizokutwa zilikuwa bidhaa bandia.

    Operesheni hiyo, iliyosababisha kukamatwa kwa bidhaa zenye thamani ya zaidi ya dola za Vietnam bilioni 2 sawa na dola za Marekani 76,053, ilikuwa sehemu ya kampeni dhidi ya biashara haramu ambayo imeendelea kushamiri waziwazi kwa miongo kadhaa.

    Takriban kilomita 30 kutoka eneo hilo, katika soko la bidhaa za mitumba lililopo katika kitovu cha utalii cha Ho Chi Minh, aina hizo hizo za ndala bandia, zinazoiga bidhaa ambazo huuzwa kwa hadi dola 900 katika masoko ya kimataifa, zinauzwa kwa dola 57 kwa jozi.

    Kando yake kuna bidhaa nyingine nyingi bandia, zikiwemo mikoba yenye chapa ya "Chanel", fulana za "Prada" na saa za "Rolex" zilizopangwa kwenye vibanda vya soko.

    Vietnam inatambulika duniani kama mojawapo ya vituo vikuu vya bidhaa bandia za bei nafuu, hasa bidhaa za kifahari za wabunifu maarufu, na ina baadhi ya masoko makubwa zaidi ya bidhaa hizo duniani.

    Sasa, huku ikikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, serikali ya Vietnam imeanzisha kampeni ya kuondoa sifa hiyo.

    Mnamo tarehe 7 Mei, serikali ilianzisha operesheni ya kitaifa dhidi ya bidhaa na shughuli zinazokiuka haki za umiliki wa ubunifu, ikiwemo utengenezaji na uuzaji wa bidhaa bandia, uharamia wa maudhui mtandaoni na ukiukaji wa alama za biashara.

  2. Nigeria yasema raia wake wawili wameuawa Afrika Kusini huku mashambulizi dhidi ya wahamiaji yakiongezeka

    Muandamanaji

    Chanzo cha picha, EPA

    Nigeria imesema kuwa raia wake wawili wameuawa nchini Afrika Kusini "wakati ambapo raia wa kigeni wanaendelea kulengwa isivyo haki" nchini humo.

    Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria ilisema kuwa Emeka Charles Iroegbu aliuawa tarehe 28 Juni, akidaiwa kufariki mikononi mwa maafisa wa polisi waliotumia "mbinu za kikatili za mahojiano". Pia ilisema kuwa mmiliki wa duka, Musa Yunana Joe, aliuawa siku hiyo hiyo na watu wasiojulikana.

    Hadi sasa, mamlaka za mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria, hazijatoa tamko kuhusu matukio hayo.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria ilisema kuwa matukio haya yanatokea wakati ambapo hisia za kupinga wahamiaji zinaongezeka nchini Afrika Kusini.

    Hali hiyo imesababisha takribani raia 25,000 kutoka mataifa mengine ya Afrika kurejeshwa katika nchi zao, wakiwemo takribani Wanigeria 700.

    Waandamanaji nchini Afrika Kusini wamekuwa wakiiomba serikali kuchukua hatua zaidi kudhibiti uhamiaji haramu. Wanasema kuwa raia wa kigeni wanachukua nafasi za ajira na kunufaika isivyo haki na huduma za umma.

    Nigeria pia imesema itadai fidia kutoka kwa Afrika Kusini kwa raia wake walioondoka nchini humo, ikiongeza kuwa serikali ya Abuja imeanza kuorodhesha biashara na mali zilizotelekezwa na Wanigeria.

    Hata hivyo, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ijumaa, Waziri wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Kusini, Khumbudzo Ntshavheni, alisema serikali yake haitalipa fidia na kwamba Wanigeria wanaweza kuuza mali zao zilizosajiliwa walizoacha nchini humo katika soko la Afrika Kusini.

    Unaweza kusoma;

  3. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu leo