Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran yasema inafanya mazungumzo na Oman lakini si na Marekani

Iran inasema inafanya mazungumzo na Oman kufikia "makubaliano" kuhusu njia ya muda kupitia Lango la Hormuz ili kuruhusu usafirishaji wa kibiashara kurejea.

Moja kwa moja

Seif Abdalla

  1. Chama cha muungano nchini Afrika Kusini kimefungua kesi mahakamani kupinga sheria iliyomkasirisha Trump

    Chama cha Democratic Alliance cha Afrika Kusini, ambacho ni chama cha pili kwa ukubwa katika muungano unaounda serikali, kilifungua kesi mahakamani siku ya Jumatatu kupinga sheria ya kutaifisha ardhi; sheria ambayo Rais wa Marekani Donald Trump aliirejelea alipositisha misaada kwa nchi hiyo mwaka jana.

    Kesi hiyo imezua mvutano na chama kikubwa zaidi, African National Congress, wakati nchi hiyo ikijiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Novemba.

    Sheria ya Kutaifisha Ardhi (Expropriation Act) inaruhusu serikali kuchukua ardhi kwa ajili ya maslahi ya umma—katika baadhi ya matukio bila kumlipa mmiliki fidia—ikiwa ni sehemu ya juhudi za kushughulikia athari za mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid).

    Imekuwa mada ya mjadala mrefu na mara nyingi wenye mvutano mkali kwa miaka mingi, na ikapitishwa kuwa sheria na Rais Cyril Ramaphosa mnamo Januari 2025. Hakuna ardhi iliyochukuliwa hadi sasa.

  2. EU yataka mipaka imara zaidi kufuatia wahamiaji kuvuka kuingia Ceuta

    Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, ametoa wito wa "hatua za pamoja" kuhusu usalama wa mipaka kufuatia wimbi la vurugu la makumi ya maelfu ya wahamiaji walioingia kutoka Morocco hadi eneo la Uhispania la Ceuta wiki iliyopita.

    Uhispania inakadiria kuwa takriban wahamiaji 69,500 sasa wamerejea Morocco, idadi inayozidi makadirio ya awali ya watu 50,000. Idadi rasmi ya vifo upande wa Uhispania wa mpaka ni 72, huku vifo 11 vikiripotiwa upande wa Morocco.

    Siku ya Jumanne, mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya (EU) watafanya mazungumzo ya dharura kwa njia ya video ili kujadili suala hilo.

    Matukio hayo huko Ceuta yameleta mvutano katika mahusiano kati ya baadhi ya nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya.

    Katika barua aliyomwandikia Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sánchez, von der Leyen alipongeza "hatua zake za haraka" katika kushughulikia mgogoro huo.

    Hata hivyo, aliongeza kusema: "Kutokana na tukio hili, ni wazi kwamba tunapaswa kufanya zaidi ili kuimarisha mipaka yetu katika maeneo muhimu."

    Kufuatia kuvuka kwa wahamiaji hao kwenda Ceuta, Italia ilisitisha kwa muda makubaliano ya Schengen na Uhispania.

    Makubaliano ya Schengen yanaondoa ukaguzi wa mipaka na kwa sasa yanahusisha zaidi ya watu milioni 450 na nchi 29 barani Ulaya

  3. Urusi yasema watu saba wameuawa na 40 kujeruhiwa baada ya droni ya Ukraine kushambulia ufukwe wenye watu wengi

    Mamlaka za eneo hilo zimesema kuwa ndege isiyo na rubani (drone) ilianguka kwenye ufukwe wenye watu wengi kusini mwa Urusi, na kuua watu saba wakiwemo watoto watatu.

    Katika picha za mitandao ya kijamii zilizothibitishwa na BBC, ndege hiyo inaonekana ikielekea kwa kasi kwenye eneo la miamba kabla ya kuanguka na kulipuka na kuwa mpira wa moto kwenye ufukwe uliopo chini, huku watalii wakishuhudia tukio hilo wakiwa ukingoni na ndani ya maji.

    Gavana wa eneo la Krasnodar, Veniamin Kondratyev, alisema kuwa jumla ya watu waliojeruhiwa ilifikia 40, huku watu 17 wakipelekwa hospitalini.

    Aliishutumu Ukraine kwa kufanya "shambulio la makusudi dhidi ya raia". Ukraine haijatoa tamko lolote. Pande zote mbili zinakanusha kulenga raia kwa makusudi.

    Haijulikani wazi ni nini kilikuwa lengo la ndege hiyo. Baadhi ya chaneli za Telegram za Ukraine zimedai kuwa ilianguka ufukweni kutokana na vita vya kielektroniki vilivyovuruga mawimbi ya mawasiliano ya ndege hiyo. Vyombo vya habari vya Urusi vilinukuu mashuhuda kadhaa wakisema kuwa milio ya risasi ilisikika kabla ya mlipuko huo, jambo linaloashiria kuwa mifumo ya ulinzi wa anga huenda ilijaribu kuitungua ndege hiyo.

    Ajali hiyo ilitokea kwenye ufukwe karibu na kijiji cha Arkhipo-Osipovka katika Bahari Nyeusi. Kutokana na hali ya hewa ya joto, ufukwe mrefu na miundombinu bora ya utalii, eneo hilo ni maarufu kwa Warusi wanaokwenda likizoni, hasa tangu vikwazo vilipopunguza uwezekano wa kusafiri nje ya nchi kwa watu wengi.

    Watalii na wakazi wa Arkhipo-Osipovka waliambia vyombo vya habari vya eneo hilo kuwa hakuna ving'ora vilivyolia kabla ya shambulio hilo la ndege isiyo na rubani.

    "Tulijikinga kwa kutumia viti vya kupumzikia ufukweni, na hatukuona ilipolipukia," alisema mtalii mmoja. Mtu mwingine alisema kuwa ingawa hakuona ndege hiyo ikigonga, alisikia "milio ya risasi, kama ya bunduki ya rashasha" ikifuatiwa na mlipuko.

  4. Ripoti za shambulio dhidi ya meli ya kibiashara karibu na Mlango Bahari wa Hormuz

    Shirika la Uingereza la Operesheni za Biashara ya Baharini (UKMTO) limetangaza kuwa limepokea taarifa kuhusu mkasa wa baharini uliotokea maili 20 za baharini kaskazini mashariki mwa Al Khasab, Oman.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, meli ya mizigo ilitoa taarifa kupitia njia ya mawasiliano ya dharura ya VHF 16 kwamba ilikuwa imelengwa na kitu kisichotambulika.

    Tovuti inayofuatilia mikasa ya ajali baharini ilisema kuwa "mamlaka zinafanya uchunguzi kuhusu tukio hilo."

    Jana, meli ya kubeba mafuta katika eneo hilo iliripoti mlipuko uliotokea karibu nayo, lakini kwa mujibu wa Shirika la Operesheni za Biashara ya Baharini, wafanyakazi na sehemu ya nje ya meli hiyo hawakupata madhara.

  5. Iran: Tulikuwa tayari kushambulia Ukraine, lakini tulisitisha shambulio hilo baada ya nchi hiyo kuomba radhi

    Aliyekuwa kamanda wa IRGC, Mohsen Rezaei, alisema katika mahojiano mapya ya televisheni kwamba vikosi vya jeshi la Iran vilikuwa tayari kushambulia maeneo matatu nchini Ukraine baada ya Ukraine kushambulia meli ya kibiashara ya Iran katika Bahari ya Caspian, lakini uamuzi huo ulisitishwa kufuatia kile alichokiita "omba-radhi" kutoka Ukraine.

    Bw. Rezaei anarejelea mazungumzo ya simu kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Ukraine, ambapo, kulingana na Abbas Araghchi, mwenzake wa Ukraine, Kiev ilisema kuwa hakukuwa na nia ya kushambulia meli ya kibiashara ya *Anna* katika Bahari ya Caspian na kwamba hatua hiyo ilichukuliwa kama sehemu ya vita dhidi ya Urusi, na si kama njia ya kuchochea mvutano zaidi na Tehran.

    Bw. Rezaei, ambaye ni mshauri mkuu wa kijeshi wa kiongozi wa Iran, alidai katika mahojiano hayo kwamba katika siku za mwisho za vita vya siku 40, "mashambulizi sahihi zaidi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Iran dhidi ya kambi za Marekani"—ambayo kwa maoni yake yalisababisha "kambi ya Kuwait kuharibiwa vibaya," vikosi vya Marekani "kuondoka Erbil, Iraq," na "kuhamishwa kwa makamanda wa CENTCOM kutoka Jordan hadi Israel"—yalikuwa mambo yaliyozuia shambulio la ardhini la Marekani.

    Bw. Rezaei, ambaye aliongoza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (Revolutionary Guard) wakati wa vita kati ya Iran na Iraq, alizungumzia mwelekeo wa sasa wa vita vya nchi hiyo na Marekani katika Lango la Bahari la Hormuz akisema: "Hatutaruhusu njia yoyote isiyo ya Iran kufunguliwa katika Lango la Bahari la Hormuz.

    Hata kama Marekani italeta meli katika njia hiyo ni haramu kupitia Lango la Bahari la Hormuz, tutailenga meli hiyo."

  6. Iran yasema inafanya mazungumzo na Oman na si Marekani, baada ya Trump kusema mazungumzo yataanza tena

    Iran inasema inafanya mazungumzo na Oman ili kufikia "makubaliano" kuhusu njia ya muda kupitia Lango la Bahari la Hormuz, ili kuruhusu usafirishaji wa kibiashara kurejea.

    Taarifa hiyo ilitolewa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema kuwa mazungumzo mapya ya kumaliza uhasama na Iran yangeanza siku ya Jumatatu - na kwamba alikuwa amesitisha mashambulizi makubwa dhidi ya nchi hiyo kwa ajili ya lengo hilo.

    Trump hakutaja ni nani watakaoshiriki katika mazungumzo hayo. Hata hivyo, Iran ilisema haifanyi mazungumzo na Marekani - na haina mpango wa kufanya hivyo.

    Kukanusha huko kwa Tehran inaonekana kulimkasirisha rais wa Marekani, ambaye baadaye aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social kwamba uongozi wa Iran una "tabia ya unafiki wa hali ya juu".

    Akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House baadaye, alisisitiza kuwa mazungumzo hayo yanaendelea.

    "Yanaendelea hivi sasa... hii ni fursa ya mwisho kwao kutia saini makubaliano mazuri," alisema.

    Mwishoni mwa wiki, Trump alikuwa amesema kuwa "misingi" ya makubaliano ilikuwa imekubaliwa - na ingejumuisha kufunguliwa tena kwa Hormuz, njia muhimu ya maji ambayo kufungwa kwake na Iran kumesababisha bei ya mafuta kupanda kwa kasi.

    Tehran imefunga njia hiyo mara kwa mara tangu Marekani na Israel zilipoanza mashambulizi dhidi ya nchi hiyo mwezi Februari.

  7. Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja