Serikali ya Tanzania yasema kukatika kwa umeme Jumamosi kulizuia janga kubwa zaidi
Serikali ya Tanzania imesema kukatika kwa umeme nchini kote siku ya Jumamosi kulisababishwa na mfumo wa kiotomatiki wa usalama wa Gridi ya Taifa, ambao ulijizima ili kuzuia uharibifu mkubwa zaidi wa mtandao wa umeme.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Gridi ya Taifa imewekewa mifumo ya kisasa ya kidijitali ya ulinzi ambayo hujitenga au kuzima sehemu za mtandao moja kwa moja inapobaini hitilafu kubwa.
Amesema teknolojia hiyo imeundwa kuzuia kusambaratika kwa mfumo mzima wa umeme na kulinda miundombinu muhimu.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya hitilafu ya kiufundi kwenye Gridi ya Taifa kusababisha kukatika kwa umeme katika maeneo yote yaliyounganishwa na gridi hiyo.
Hitilafu hiyo iliathiri shughuli za biashara, usafiri, mawasiliano na huduma nyingine muhimu kwa saa kadhaa, huku maelfu ya wananchi wakikumbwa na usumbufu katika shughuli zao za kila siku.
Kwa mujibu wa Msigwa, hatua ya mfumo kujizima moja kwa moja inaonesha kuwa miundombinu ya umeme ya Tanzania imejengwa kwa teknolojia za kisasa zenye uwezo wa kubaini hitilafu na kuchukua hatua za haraka bila kusubiri uingiliaji wa kibinadamu.
Hata hivyo, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Umeme na Nishati kuunda kamati ya uchunguzi kubaini chanzo cha hitilafu hiyo na kupendekeza hatua za kuzuia tatizo kama hilo kujitokeza tena.
TANESCO imetakiwa kuwasilisha taarifa ya awali ndani ya wiki moja ili kuiwezesha serikali kuchukua hatua stahiki, huku uchunguzi wa kina ukiendelea.
Soma Zaidi: