Moja kwa moja, Iran na Marekani zakubaliana kusitisha mashambulizi na kufanya mazungumzo Doha - Axios

Kwa mujibu wa Axios Marekani na Iran zinatarajiwa kukutana mjini Doha siku ya Jumanne kutafuta suluhu ya tofauti zao kuhusu Mlango wa Hormuz.

Muhtasari

Iran na Marekani zakubaliana kusitisha mashambulizi na kufanya mazungumzo Doha - Axios

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Rais wa Shirikisho la Soka Saudi Arabia ajiuzulu baada ya timu kutolewa Kombe la Dunia

    m

    Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    Rais wa Shirikisho la Soka la Saudi Arabia, Yasser Al Mashal, amejiuzulu kufuatia kutolewa kwa timu ya taifa ya nchi hiyo katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.

    Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Al Mashal amesema kutofuzu kwa timu hiyo kwenda hatua inayofuata ya mashindano hayo ni matokeo ambayo hayaendani kwa namna yoyote na matarajio na malengo ya taifa hilo.

    "Kutofuzu kwa timu ya taifa kwenda hatua inayofuata ya Kombe la Dunia ni matokeo yasiyoendana na matarajio yetu," aliandika Al Mashal kwenye mitandao ya kijamii.

    "Ninabeba jukumu kamili kwa matokeo haya na naomba radhi kwa wote waliotarajia kuiona timu yetu ikifanya vizuri zaidi.

    Kwa kuamini kwamba uwajibikaji unahitaji kutoa nafasi kwa mwanzo mpya, nimeamua kutoendelea hadi mwisho wa muhula wangu wa uongozi."

    Saudi Arabia ilimaliza mkiani mwa Kundi H ikiwa na pointi mbili, baada ya kutoka sare dhidi ya Uruguay na Cape Verde na kupoteza mechi dhidi ya Hispania.

    Al Mashal alikuwa ameongoza Shirikisho la Soka la Saudi Arabia kwa miaka saba na alihusika kwa kiasi kikubwa katika jitihada zilizoiwezesha Saudi Arabia kupata haki ya kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la mwaka 2034.

    Saudi Arabia ilikuwa ikishiriki Kombe la Dunia kwa mara ya tatu mfululizo na mara ya saba kwa ujumla. Hata hivyo, maandalizi yake yaliathiriwa na uamuzi wa kumwondoa kocha Herve Renard na kumteua Georgios Donis chini ya miezi miwili kabla ya mashindano kuanza.

    Soma pia:

  2. WHO: Vifo 1,300 Ulaya vyahusishwa na wimbi kali la joto

    F

    Chanzo cha picha, EPA

    Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema wimbi la joto lisilo la kawaida linaloikumba Ulaya huenda limesababisha vifo vya ziada vya zaidi ya watu 1,300 tangu Juni 21.

    Rekodi za viwango vya joto zimeendelea kuvunjwa katika mataifa kadhaa ya Ulaya, yakiwemo Ujerumani, Poland na Jamhuri ya Czech, huku wimbi hilo la joto kali likiendelea kuelekea mashariki mwa bara hilo.

    Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Tedros alisema joto kali mara nyingi huitwa "muuaji kimya" kwa sababu linaweza kusababisha vifo bila dalili za wazi.

    Aliongeza kuwa nyumba, maeneo ya kazi na shule nyingi barani Ulaya hazikujengwa kuhimili viwango hivyo vya juu vya joto.

    Wizara ya Afya ya Ufaransa imesema takriban vifo 1,000 zaidi ya vilivyotarajiwa vimerekodiwa nchini humo tangu Jumatano, huku idadi kubwa ya vifo hivyo ikiwa ni ya watu wenye umri wa miaka 65 na kuendelea.

    WHO imeonya kuwa Ulaya ndiyo bara linaloongezeka joto kwa kasi zaidi duniani, kwa kiwango cha mara mbili ya wastani wa ongezeko la joto duniani.

    "Mamilioni ya watu barani Ulaya kwa sasa wanaishi chini ya wimbi kali la joto, mamia wamefariki, shule zimefungwa na mifumo ya usambazaji umeme iko chini ya shinikizo kubwa," alisema Tedros.

    Soma Zaidi:

  3. Iran na Marekani zakubaliana kusitisha mashambulizi na kufanya mazungumzo Doha - Axios

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Axios imeripoti kuwa Tehran na Washington zimekubaliana kusitisha mashambulizi katika Ghuba ya Uajemi na kufanya mazungumzo ya moja kwa moja katika siku chache zijazo mjini Doha, Qatar.

    Mwandishi wa Axios, Barak Ravid, aliandika Jumapili jioni kwamba afisa mmoja mwandamizi wa Marekani amesema Marekani na Iran zimekubaliana kuacha kushambuliana, na kwamba pande hizo mbili zinatarajiwa kukutana mjini Doha siku ya Jumanne kutafuta suluhu ya tofauti zao kuhusu Mlango wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa Axios, mazungumzo hayo yataangazia zaidi suala la Mlango wa Hormuz.

    Iran imehusisha mapigano mapya na Marekani na kile inachodai kuwa ni kuingilia usimamizi wake wa Mlango wa Hormuz.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema wakati wa ziara yake nchini Iraq kwamba kufunguliwa kikamilifu kwa Mlango wa Hormuz, kwa mujibu wa makubaliano na Marekani, ni jukumu la Tehran pekee, na kwamba kuingilia mchakato huo kutavuruga juhudi hizo na kuongeza mvutano katika eneo hilo.

    Maelezo zaidi:

  4. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 29 Juni 2026.