Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Marekani, Israel na Iran vinaonyesha kuwa sheria za kimataifa za vita zimekiukwa
Mashambulizi ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran, katika miundombinu ya nishati ya nchi hiyo, pamoja na vitendo vya kulipiza kisasi vya Tehran dhidi ya majirani zake wa Ghuba ya Uajemi, vyote vinaonyesha kwamba kanuni za kimataifa juu ya vita zimebadilika.
Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kutumia "nguvu kali na kubwa" kushambulia vituo vya nishati vya Iran. Wiki iliyopita, alisema "ataharibu kwa kiwango kikubwa" kiwanda cha gesi cha South Pars ikiwa Iran itashambulia tena vituo vya nishati vya Qatar.
Pia ameweka tarehe ya mwisho, akionya kwamba ikiwa viongozi wa Iran hawatafungua Mlango wa Bahari wa Hormuz, Marekani "itaharibu mitambo mbalimbali ya umeme ya Iran, kwa kuanzia na ile mikubwa."
Luis Moreno-Ocampo, mwendesha mashtaka mkuu wa kwanza wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), anasema sheria za kimataifa ziliundwa ili kuwalinda raia na kuzuia nchi kuanzisha vita isipokuwa kwa kujilinda au kwa idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Ameiambia BBC vita dhidi ya Iran, kulingana na sheria za kimataifa, ni "uhalifu dhidi ya amani."
Bw. Moreno-Ocampo pia amesisitiza kwamba vitisho vya Donald Trump vya kushambulia mitambo ya umeme ya Iran, kama vile mashambulizi ya Iran na Israel dhidi ya miundombinu ya nishati, haviingii ndani ya mfumo halali wa mashambulizi ya kijeshi.
Analinganisha vitendo hivi na mashambulizi ya Urusi kwenye vituo vya nishati vya Ukraine, ambayo yalisababisha maafisa wa Urusi kushtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kwa uhalifu wa kivita.
"Vitendo vya Urusi nchini Ukraine, au vitendo vya Marekani nchini Iran na Venezuela, vyote vinaangukia ndani ya kile kinachoitwa 'uhalifu dhidi ya amani.' Ni matumizi ya nguvu za kijeshi na nchi moja dhidi ya uhuru, uadilifu wa eneo, au uhuru wa kisiasa wa nchi nyingine," anasema.
"Sasa tumehama kutoka kufuata sheria hadi maamuzi kutokana na uhuru wa mtu binafsi; chochote Rais Trump anachoamua leo kinakuwa sheria. Dunia kama hiyo si endelevu."
Marekani yajibu
Ikulu ya White House imejitaza kauli za Moreno-Ocampo kuwa za "ujinga" na kusema kwamba Trump anachukua "hatua kali ili kuondoa tishio la utawala hatari na wa kigaidi."
Afisa wa Ikulu ya Marekani aliongeza kwamba mauaji ya rai "mikononi mwa utawala wa Iran" katika nchi hiyo yanaonesha "umuhimu wa hatua za rais."
Akijibu wasiwasi kwamba kushambulia mitambo ya umeme ya Iran kunaweza kuwa uhalifu wa kivita, Mike Waltz, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, aliiambia CBS: "Unapokuwa na utawala unaodhibiti sehemu kubwa ya miundombinu muhimu na kuutumia kuwakandamiza watu wake, kushambulia majirani zake na kuendeleza mpango wa nyuklia kinyume na vikwazo vya Umoja wa Mataifa, hayo ni mashambulio halali."
Moreno-Ocampo anasema mashambulizi ya Iran dhidi ya majirani zake wa Ghuba ya Uajemi, nchi ambazo hazijashambulia Iran, pia ni "uhalifu dhidi ya amani" chini ya sheria za kimataifa.
Marekani, Israel na Iran si wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Hata hivyo, utawala wa Trump umewawekea vikwazo majaji wake kadhaa kutokana na uchunguzi wa awali wa mahakama hiyo kuhusu Marekani na Israel.
Luis Moreno-Ocampo anasema chini ya Mkataba wa Roma, ambao ndio msingi wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo, "kushambulia kimakusudi maeneo ya kiraia ... kunafafanuliwa kuwa ni uhalifu wa kivita.”
Bila shaka, ikiwa maeneo ya kiraia yatatumika kwa madhumuni ya kijeshi, yanaweza kupoteza ulinzi wa kisheria, lakini hata katika hali kama hiyo, mashambulizi lazima yazingatie kanuni za sheria za kimataifa za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kutofautisha kati ya raia na vikosi vya kijeshi.
Makundi ya haki za binadamu yanaonya kwamba mashambulizi dhidi ya mitambo ya umeme ya Iran yanaweza kuwa na athari mbaya kwa maisha ya raia, hasa kwa vile Wairani tayari wanakabiliwa na kukatika kwa umeme, na umeme ni muhimu kwa ajili ya kusukuma maji majumbani.
Iran imesema itashambulia miundombinu ya nishati na maji ya majirani zake wa Ghuba ikiwa Marekani itafanya shambulio kama hilo.
Wakati wa vita, makombora pia yametua karibu na vituo vya nyuklia nchini Iran na Israel. Shirika la Afya Duniani limetangaza mzozo huo kuwa katika "hatua hatari" na kutoa wito wa kujizuia.
Brian Finucane, wakili wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ameiambia BBC ikiwa Donald Trump atatekeleza vitisho vyake dhidi ya vituo vya nishati vya Iran, "ni vigumu kuona jinsi shambulio kama hilo linavyoweza kuwa halali."
Kiwango cha uharibifu
Mashambulizi ya anga ya Israeli yamelenga vituo kadhaa vya mafuta ndani na karibu na Tehran, na kusababisha moto mkubwa na moshi kupanda angani.
Iran pia imelenga miundombinu ya nishati nchini Qatar, Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Bahrain, Kuwait, Oman, Iraq na Israel. Shirika la Kimataifa la Nishati linasema vituo 40 vya nishati katika nchi tisa vimeharibiwa vibaya tangu vita kuanza.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani mashambulizi ya Iran dhidi ya majirani zake wa Ghuba, lakini wakosoaji wanasema kulaani ukiukaji wa sheria za kimataifa wa Iran kunapoteza maana wakati Marekani inajitenga waziwazi na kanuni hizo.
Brian Katulis, afisa wa zamani wa usalama wa taifa wa Marekani, anasema, “vitisho na hatua za Marekani dhidi ya miundombinu ya nishati nchini Iran na Venezuela vinatuma ujumbe kwamba "unaweza kufanya chochote unachotaka. Sheria ya msituni imerejea.."
Katulis pia anaamini kutoweza kwa Trump kujenga muungano mzuri ili Mlango-Bahari wa Hormuz ufanye kazi ni matokeo ya moja kwa moja ya kupungua kwa imani ya washirika wa Marekani.
Anasema serikali ya Marekani iko katika enzi ya "diplomasia ya kulazimisha."
Ikulu ya White House imekanusha madai hayo. Afisa mmoja anasema Trump ameirejesha nafasi ya Marekani kama taifa lenye nguvu zaidi duniani ili kuilinda na washirika wake kutokana na tishio la Iran.
Aliongeza: "Marais waliopita walitumia miaka 47 wakizungumzia kuhusu tishio la Iran, lakini hawakuchukua hatua, badala yake waliruhusu utawala huu wa kigaidi kupanua uwezo wake wa uharibifu."