Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Saudi Arabia iko njia panda ikiwa katika juhudi za kujiweka mbali na vita vya Iran
Tangu Marekani na Israel zilipoanzisha vita dhidi ya Iran tarehe 28 Februari, Saudi Arabia kwa kiasi kikubwa imejitahidi kuepuka kujihusisha moja kwa moja na mzozo huo.
Lakini sasa, baada ya kushambuliwa kutoka pande tatu, Saudi Arabia inaonekana imefikia mwisho wa uvumilivu wake.
Wiki hii, ilifanya mashambulizi ya pamoja na Marekani dhidi ya makundi ya wanamgambo yanayoungwa mkono na Iran nchini Iraq, ambayo inaamini yamekuwa yakirusha ndege zisizo na rubani kushambulia ufalme huo.
Kwa Saudi Arabia, mtanziko uliopo sasa ni kama iendelee kujibu mashambulizi hayo ili kuzuia mengine yasitokee, au ijaribu kupunguza mvutano, huenda kwa kufanya mazungumzo au kutoa motisha kwa baadhi ya wapinzani wake.
Kwa hiyo, ni nani anayemshambulia nani, na kwa nini?
Kwanza, ni muhimu kuelewa muktadha.
Kwa ujumla, kuna pande mbili kuu katika mzozo ambao umekuwa ukiikumba Ghuba ya Uajemi na maeneo mengine ya Mashariki ya Kati kwa kipindi cha miezi mitano sasa.
Upande mmoja upo Iran pamoja na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Washirika wao ni pamoja na Waouthi wa Yemen, kundi la kikabila lililochukua udhibiti wa sehemu kubwa ya Yemen mwaka 2014.
Pia Iran inaunga mkono Vikosi vya Uhamasishaji nchini Iraq, kundi la wanamgambo linalodaiwa kufanya mashambulizi 30 ya ndege zisizo na rubani dhidi ya Saudi Arabia, na ambalo sasa limejibiwa kwa kushambuliwa.
Aidha, kuna Hezbollah nchini Lebanon, ambalo bado ni kundi lenye nguvu, ingawa kwa sasa limepunguza shughuli zake na linaonekana kujizuia kushiriki moja kwa moja katika mapigano.
Upande wa pili wa mzozo huu upo Marekani, ikiwa na vikosi vyake vyenye nguvu vya Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM), pamoja na kwa viwango tofauti vya ushiriki, nchi za Kiarabu za Ghuba na Jordan.
Israel inaendelea kuwa mshirika wa karibu wa Marekani, lakini kwa sasa haishiriki moja kwa moja katika vita hivi.
Hivi karibuni, Iran imeelekeza mashambulizi yake ya ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya Jordan, Kuwait na Bahrain. Pia imelenga meli za kibiashara zinazojaribu kupita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz bila kufuata sheria na njia mpya zilizowekwa na Iran.
Kushiriki kwa makundi ya wanamgambo wa Iraq na Waouthi wa Yemen ni jambo jipya kwa kiasi fulani. Hali hiyo inaonesha kwamba, bila kufikiwa kwa makubaliano ya kudumu ya amani kati ya Marekani na Iran, eneo hilo lina hatari ya kuzama zaidi katika mzozo unaozidi kupanuka.
Kuna sababu kadhaa zinazofanya Saudi Arabia ijitahidi kuepuka kuingia katika vita vya kiwango kikubwa.
Mtawala wake wa facto, Mwanamfalme Mohammed bin Salman, ambaye ni kijana kwa kulinganisha na viongozi wengi wa eneo hilo, ameanzisha mpango wa maendeleo unaojulikana kama "Dira ya 2030."
Lengo lake ni kuifanya Saudi Arabia ipunguze utegemezi wake wa mapato ya mafuta na kujenga sekta mbalimbali za kisasa za uzalishaji na huduma ambazo zitatoa ajira zenye tija kwa mamia ya maelfu ya wahitimu wa vyuo na shule wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka.
Sehemu ya mpango wa Vision 2030 ni kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi.
Pia unahusisha ujenzi wa miundombinu kama vile vituo vya kuhifadhi na kuchakata data , ambavyo vinaweza kuwa rahisi kushambuliwa wakati wa migogoro ya kijeshi.
Hali hii haiwezi kufanikiwa ikiwa Saudi Arabia itajikuta ikikabiliwa na tishio la kudumu la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani zinazorushwa na Waouthi kutoka mpaka wake wa kusini nchini Yemen au makombora ya masafa marefu yanayorushwa moja kwa moja na Iran.
Mnamo Septemba 2019, Saudi Arabia ilikumbwa na mshtuko mkubwa.
Wakati huo, uhusiano kati ya Saudi Arabia na Iran ulikuwa mbaya, na Wasaudia waliamka na kugundua kuwa kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran nchini Iraq lilikuwa limerusha ndege zisizo na rubani dhidi ya vituo viwili muhimu vya mafuta vya Saudi Arabia, vya Abqaiq na Khurais.
Wakati huo kulikuwa na madai kwamba mashambulizi hayo yalifanywa na Wahouthi wa Yemen, lakini nilitembelea eneo hilo mara baada ya tukio na niliweza kuona wazi kuwa mashimo yaliyosababishwa na mashambulizi kwenye miundombinu hiyo yalikuwa yakielekea upande wa kaskazini.
Mashambulizi hayo yalisababisha karibu nusu ya mauzo ya mafuta ya Saudi Arabia kusimama kwa siku kadhaa, na yalikuwa onyo kwa Riyadh kuhusu jinsi miundombinu yake muhimu ya kitaifa ilivyo katika hatari ya kushambuliwa.
Siku ya Jumatatu, picha za satelaiti zilionesha kuwa kituo cha mafuta cha Abqaiq kilishambuliwa tena na ndege zisizo na rubani zilizorushwa na makundi ya wanamgambo yanayoungwa mkono na Iran nchini Iraq.
Kisha kuna suala la mafuta, ambayo bado ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Saudi Arabia.
Iran ilijibu mashambulizi ya Marekani na Israel yaliyofanyika mwezi Februari kwa kufunga kwa kiasi kikubwa Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa meli kati ya Iran na Ghuba ya Uajemi, ambako takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) duniani hupitia.
Kwa kujibu hatua hiyo, Saudi Arabia iliongeza uzalishaji na usafirishaji wa mafuta kadiri ilivyoweza, takribani mapipa milioni tano kwa siku, kupitia bomba lake la mafuta linalounganisha mashariki na magharibi mwa nchi hadi kwenye kituo chake cha kusafirisha mafuta cha Yanbu, kilichopo kwenye pwani ya Bahari ya Shamu.
Kutoka huko, mafuta hayo yalipakiwa kwenye meli za mafuta ambazo zilielekea kusini, kupitia Bahari ya Arabia, na kusafirishwa kwenda masoko ya Asia.
Kwa muda, mambo yalienda vizuri.
Lakini tarehe 13 Julai, Saudi Arabia ilishambulia Uwanja wa Ndege wa Sanaa, ulioko nje kidogo ya mji mkuu wa Yemen.
Shambulio hilo lilidaiwa kufanywa na serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudi Arabia, ambayo ilisema ilitaka kuzuia ndege ya Iran kutua katika uwanja huo.
Kwa kulipiza kisasi, waasi wa Houthi walishambulia viwanja vya ndege vya Saudi Arabia vilivyoko Abha na Jizan.
Jambo lililoitia wasiwasi zaidi Riyadh ni kwamba Wahouthi wameanza pia kushambulia meli za Saudi Arabia katika Bahari ya Shamu, na kufanya safari kupitia Mlango wa Bahari wa Bab el-Mandeb, ulioko kusini mwa Bahari hiyo, kuwa hatari sana.
Hali hiyo imeathiri vibaya usafirishaji wa mafuta ya Saudi Arabia kwenda masoko ya Asia.
Saudi Arabia ilitumia miaka saba kujaribu kuwashinda Wahouthi kwa mashambulizi ya anga, lakini haikufanikiwa.
Vita vilivyopamba moto nchini Yemen vilikuwa mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu katika nyakati za kisasa, na athari zake bado zinaendelea kuonekana hadi leo.
Mwaka 2022, Saudi Arabia ilikubaliana na Waouthi kusitisha mapigano kwa makubaliano ya amani yaliyokuwa dhaifu, na kulikuwa pia na taarifa kwamba fedha zililipwa kwa baadhi ya pande husika ili kudumisha utulivu.
Hata hivyo, sasa Saudi Arabia, ambayo ndiyo nchi tajiri zaidi katika eneo hilo, kwa mara nyingine inakabiliwa na tishio la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora kutoka kwa jirani yake wa kusini, Yemen, wakati huohuo ikikabiliwa na mashambulizi yanayotoka Iraq upande wa kaskazini.
Hakuna hata moja ya hali hizi iliyotarajiwa katika mipango ya Dira ya 2030.