Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi kunguni alivyosababisha kusimamishwa kwa safari za ndege za kimataifa
Safari ya ndege ya shirika la Qantas kutoka Italia kwenda Australia iliahirishwa siku ya Jumamosi baada ya ndege hiyo kukumbwa na tatizo la kunguni.
Safari ya awali, iliyoondoka Perth, Australia, siku ya Ijumaa kuelekea Roma, Italia, ilichelewa kwa takriban saa 17, huku baadhi ya abiria wakilalamikia kuumwa na wadudu hao, gazeti la Sydney Morning Herald liliripoti.
Iliripotiwa kuwa abiria walipewa dawa za mzio ili kupunguza muwasho uliosababishwa na kuumwa huko, lakini dawa hizo ziliisha.
Ndege hiyo aina ya Boeing 787 Dreamliner imesimamishwa kufanya kazi ili kufanyiwa "usafi wa kina", msemaji wa Qantas aliliambia shirika la habari la BBC.
"Tunaomba radhi kwa wateja wetu kwa kufutwa kwa safari ya Jumamosi kutoka Roma kwenda Perth; hatua hiyo iliruhusu wahandisi na timu zetu za matengenezo kufanya usafi wa kina wa ndege hiyo baada ya tatizo kugunduliwa katika idadi ndogo ya viti," msemaji huyo alisema.
Kampuni hiyo iliongeza kuwa wateja wote walioathirika walipewa malazi na kupangiwa safari nyingine ndani ya saa 48 tangu muda wao wa awali wa kuondoka.
Kunguni hao, ambao mara nyingi hupatikana majumbani, ni vimelea vidogo visivyo na mabawa vinavyoweza kuishi kwenye nguo, samani na shuka au matandiko. Kulingana na tovuti ya Huduma ya Afya ya Taifa la Uingereza (NHS), mtu anapong'atwa na wadudu hao huwashwa , lakini kwa kawaida muwasho huo hauwezi kusababishi matatizo makubwa ya kiafya.
Hata hivyo, ni vigumu kuwaondoa wadudu hawa, na kuwatokomeza ni gharama kubwa.
Mbinu za kukabiliana na tatizo hili ni pamoja na kuosha matandiko yote, nguo, na vifaa vya nyumbani kama vile pazia kwa maji ya moto na kisha kuvikausha kwa kutumia mashine ya kufulia.
Vitu hivi vinaweza pia kuwekwa kwenye mifuko ya plastiki na kuhifadhiwa ndani ya jokofu kwa muda wa siku tatu hadi nne.
Baada ya tatizo la kunguni kwenye safari za ndege za Qantas
Chini ya wiki mbili zilizopita, tukio kama hilo liliripotiwa katika huduma kadhaa za treni zinazoendeshwa na kampuni ya Southeastern nchini Uingereza; safari hizo zilifutwa baada ya madereva kugundua wadudu hao ndani ya mabehewa ya treni zao.
Mwaka wa 2017, shirika la ndege la British Airways liliomba radhi kwa familia iliyokuwa ikisafiri kutoka Vancouver kwenda London baada ya wanafamilia hao kung'atwa na kunguni wakati wa safari ya usiku.
Shirika la ndege la Turkish Airlines nalo lilipata pigo kubwa la sifa mwaka jana baada ya gazeti la New York Times kuripoti visa kadhaa vya kunguni waliosemekana kupatikana kwenye ndege za shirika hilo.
Wakati huo, kulikuwa pia na madai kwamba shirika hilo halikuchukua hatua yoyote kushughulikia tatizo hilo.
Jinsi ya kuondoa kunguni
Inaweza kuwa vigumu kuondoa kunguni, lakini kuna hatua zinazoweza kuchukuliwa, zikiwemo:
Kufua mashuka na nguo zilizochafuliwa kwa maji ya moto na kisha kuzianika au kuzikausha mahali penye joto kali kwa angalau dakika 30.
Kuweka nguo au mashuka kwenye mfuko wa plastiki na kuviweka ndani ya jokofu kwa siku tatu au nne.
Kusafisha nyumba yako mara kwa mara - wadudu hawa wanaweza kupatikana katika maeneo safi na machafu, lakini usafi wa mara kwa mara unaweza kukusaidia kuwatambua.
Ni nini husababisha kunguni?
Kunguni mara nyingi huingia majumbani kwa kujishikiza kwenye mizigo, nguo, au samani zilizotumika.
Wanapoingia ndani, mara nyingi hujificha sehemu ambazo watu hulala, kama vile magodoro, fremu za vitanda, samani, na nyufa ndogo.
Kulingana na NHS, kuwepo kwa wadudu hawa hakusababishwi na ukosefu wa usafi, kwani wanaweza kupatikana katika nyumba zilizo safi na zile zisizo safi.
Aidha, usafi wa mara kwa mara unaweza kusaidia kugundua uwepo wao mapema.