Makubaliano ya Marekani na Iran yaibua maswali iwapo kulikuwa na haja yoyote ya vita

    • Author, Jeremy Bowen
    • Nafasi, International editor
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Makubaliano ya uelewano yaliyotiwa saini na Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian yanaweka wazi athari za kisiasa, kijeshi na kiuchumi za uamuzi uliochukuliwa bila uangalifu wa kuishambulia Iran tarehe 28 Februari.

Gharama za kibinadamu za vita hivi tayari zinaonekana wazi. Maelfu ya watu, wengi wao raia, wameuawa nchini Iran na Lebanon.

Marekani, na kwa upana wake Israel, zimepata pigo la kimkakati. Utawala wa Tehran ulikumbana na hofu yake kubwa zaidi, operesheni ya pamoja ya kijeshi iliyolenga kuudhoofisha au kuuangamiza, iliyohusisha Marekani, taifa lenye nguvu kubwa duniani, na Israel, ambayo mara nyingi huonekana kama nguvu kuu ya kijeshi Mashariki ya Kati. Hata hivyo, utawala huo haukuanguka, bali umeendelea kuimarika.

Mkakati wa Iran wa kufunga Mlango Bahari wa Hormuz, hatua ambayo ingeathiri takribani sehemu moja ya tano ya usafirishaji wa mafuta na gesi duniani pamoja na mifumo mingine muhimu ya uchumi wa kimataifa, umeilazimu Donald Trump kukubali mfululizo wa masharti ambayo yamewakasirisha na kuwatia hofu wapinzani wakali wa Iran ndani ya Marekani na serikalini Israel.

Makubaliano hayo yanapendekeza kusitishwa kwa vita nchini Lebanon. Israel inasema hilo haliwezekani na inasisitiza kuendelea na uhuru wa kijeshi nchini humo, hali ambayo inaweza kuongeza mgawanyiko kati ya Israel na Marekani na kuwanufaisha wapinzani wakali wa Iran wanaopinga maelewano yoyote na Washington.

Kwa upande mwingine, ili kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz, Marekani imekubali kuondoa mzingiro dhidi ya bandari za Iran, kusimamisha vikwazo vya kiuchumi vinavyoruhusu Iran kupata mabilioni ya dola kupitia mauzo ya mafuta, na kuanza mchakato wa kurejesha mali za Iran zilizozuiwa nje ya nchi.

Hii yote inafanyika kabla ya mazungumzo magumu kuhusu mpango wa nyuklia. Lengo ni kurejesha hali iliyokuwepo kabla ya Februari 27, siku moja kabla ya vita kuanza, ambapo mlango huo ulikuwa wazi na mazungumzo ya nyuklia kati ya Marekani na Iran yalikuwa yanaendelea.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuruhusu mazungumzo kuanza upya na meli kupita tena kupitia Hormuz.

Anthony Blinken, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika utawala wa Joe Biden, aliandika kwa mtandao wa X, kuwa mafanikio pekee ya usitishaji vita ni kufunguliwa tena kwa mlango ambao tayari ulikuwa wazi kabla ya vita, akiongeza kuwa Marekani inaonekana inalipa Iran ili kufanikisha hilo.

Swali kuhusu lengo halisi la vita hivi linaendelea kujitokeza na halitaondoka kirahisi. Wataalamu wanasema huenda hii ikawa kosa kubwa zaidi la sera za nje la Donald Trump hadi sasa.

Vita hivyo pia vinaweza kuashiria mwisho wa safari ya kisiasa ya muda mrefu ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye anakabiliwa na uchaguzi Oktoba na atahitajika kujibu maswali kuhusu mapungufu makubwa ya kiusalama katika historia ya Israel, ikiwemo kushindwa kwa vyombo vya ujasusi kugundua mpango wa Hamas wa shambulio la Oktoba 7, 2023.

Iran ilikuwa ikifahamu uwezo wake wa kufunga Hormuz, kama vile Marekani ilivyokuwa inafahamu kupitia jeshi lake na vyombo vya ujasusi.

Hata hivyo, Ali Khamenei, kiongozi wa zamani wa Iran, alikuwa na tahadhari na hakutaka kutumia mlango huo kama silaha. Baada ya kuuawa kwake na wasaidizi wake katika mashambulizi ya awali ya vita, warithi wake walichukua msimamo mkali zaidi na kuamua kuufunga mlango huo.

Hatua hiyo ilionyesha uwezo wa Iran kudhibiti njia muhimu ya uchumi wa dunia, silaha ambayo haiwagharimu sana ukilinganisha na maadui zake na hata marafiki wanaomzunguka waliotumia pesa nyingi kujenga kambi za kijeshi Mashariki ya Kati.

Isipokuwa utawala wa Assad nchini Syria, ulioporomoka mwishoni mwa mwaka 2024, kile kinachoitwa na Iran "mhimili wa upinzani" bado kipo, japo kwa kiwango cha kuyumba. Hata hivyo, umedhoofishwa sana na Israel kiasi kwamba kama bado unaweza "kupinga" au la ni jambo linaloibua mjadala usio na jibu la wazi.

Iran pia imewekeza pakubwa katika mpango wake wa nyuklia, ambao inaendelea kukanusha kuwa ni wa kutengeneza silaha za nyuklia, lakini ambao umeendelea kuwa chanzo cha hofu na shinikizo la kisiasa.

Hata hivyo, mpango huo huo umechangia kusababisha vita vilivyoiharibu Iran kwa kiwango kikubwa, licha ya utawala wake kuendelea kuwepo.

Kwa upande mwingine, kufungwa kwa Hormuz kulikuwa na athari za haraka na kubwa, na kuathiri pia nchi za Kiarabu zinazouza mafuta pamoja na uchumi wa dunia.

Jeshi la anga la Marekani na Israel lilipata ushindi wa kiufundi katika maeneo kadhaa, lakini ushindi huo haukuzuia kushindwa kwa kimkakati. Sababu kubwa ilikuwa dhana potofu kwamba kubadilisha uongozi wa Iran kungeangusha mfumo mzima wa utawala.

Hata hivyo, taasisi za Iran zimejengwa kwa miongo kadhaa kwa namna ya kustahimili jaribio la kuanguka.

Haikuwa kama Venezuela, udikteta wa rushwa katika Amerika ya Kusini, uliosambaratika baada ya kiongozi wake kutekwa na kufikishwa mahakamani nchini Marekani. Utawala wa Iran bila shaka una sifa za rushwa na ukandamizaji mkubwa, ambapo maelfu ya waandamanaji waliuawa katika mitaa ya Iran mwezi Januari. Hata hivyo, pia unategemea itikadi, imani za kidini, na mtazamo wa usalama wa taifa, shahada ya kujitolea kufa na kuishi, pamoja na fikra za uhai na uthabiti zilizoimarika kutokana na vita vya maangamizi dhidi ya Iraq ya Saddam Hussein katika miaka ya 1980.

Wakati vita vilipoanza, Rais Donald Trump alisema kwamba utawala wa Tehran ungeanguka. Aliwaambia wananchi wa Iran wajitayarishe kwa kile alichokiita fursa ya karne moja kurejesha nchi yao. Muda mfupi baadaye, alitoa wito wa kujisalimisha bila masharti.

Netanyahu, ambaye alikuwa amejaribu mara kwa mara bila mafanikio kuwashawishi watangulizi wa Trump katika Ikulu ya Marekani waingie vitani dhidi ya Iran, alitumia lugha ya kidini na ya Biblia kuelezea ukubwa wa kile alichoamini kinakaribia kutokea, akisema: "Muungano huu wa nguvu unaturuhusu kufanya kile ambacho nimekitamani kwa miaka 40: kuuangamiza utawala wa ugaidi kabisa."

Hata hivyo, hakuna kati ya viongozi hao wawili aliyefanikisha malengo yake.

Makubaliano haya si ya mwisho, bali ni mwanzo wa mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Yamejumuisha pia ahadi za awali za kuondoa vikwazo iwapo mazungumzo yataendelea vizuri.

Hatima ya mazungumzo ya siku 60 itategemea uaminifu mdogo kati ya pande zote mbili, huku upinzani kutoka kwa makundi ya msimamo mkali Tehran, Washington na Israel ukiendelea kuwa tishio.

Iran inaweza pia kuendeleza madai makubwa kupita kiasi na kuhatarisha faida za kiuchumi zinazoweza kuisaidia kuimarisha uchumi wake uliodhoofika.

Hata hivyo, makubaliano haya yanaonekana kuwa chaguo bora kuliko vita vilivyosababisha vifo vya maelfu na kuhatarisha uchumi wa dunia.

Iwapo makubaliano ya nyuklia yatakamilika kwa mafanikio na pande zote zitaheshimu ahadi zao, Mashariki ya Kati inaweza kubadilika kwa kiasi kikubwa. Lakini hilo bado ni hali ya "iwapo" kbaada ya mazungumzo mapana na magumu.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid