Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tunachojua kuhusu mashambulizi mapya kati ya Marekani na Iran
Jeshi la Marekani limesema lilifanya mashambulizi ambayo limeyataja kuwa ya "kujilinda" dhidi ya Iran, baada ya Iran kurusha makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani zilizolenga meli na nchi za Ghuba.
Mashambulizi hayo yalifanyika kwenye Kisiwa cha Qeshm, kilichopo katika Mlango wa Bahari wa Hormuz. Kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM), yalikuwa "jibu kwa majaribio ya Iran ya kuanzisha mashambulizi kote Mashariki ya Kati."
Kwa upande wake, Iran ilisema ilirusha makombora na droni dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani na helikopta zake katika "nchi moja ya eneo hilo," ikidai kuwa ilikuwa ni hatua ya kulipiza kisasi.
CENTCOM ilisema Tehran ilirusha makombora mawili kuelekea Kuwait na mengine matatu kuelekea Bahrain, lakini yote yaliharibika angani au yalidunguliwa kabla ya kufikia malengo yake.
Mashambulizi haya ya hivi karibuni yanatokea wakati mazungumzo ya kusitisha mapigano yamekwama, baada ya juhudi za kumaliza miezi kadhaa ya mapigano kushindwa kuleta maendeleo yoyote mwishoni mwa wiki.
CENTCOM pia ilisema kuwa shambulio la Kisiwa cha Qeshm lililenga kituo cha ardhini kinachotumiwa na vikosi vya Iran kuongoza na kuratibu operesheni za kijeshi. Aidha, jeshi la Marekani lilisema lilidungua ndege tatu za kivita za Iran ambazo zilikuwa zikilenga meli za kiraia zilizokuwa zikisafiri kihalali katika maji ya eneo hilo.
Jeshi la Iran (IRGC) limesema kwamba, "kuvuruga usalama wa Mlango wa Bahari wa Hormuz kutazigharimu vikosi vamizi vya Marekani kwa kiasi kikubwa."
CENTCOM pia ilisema kuwa Iran ilirusha makombora kadhaa ya balistiki kuelekea nchi za eneo hilo. "Makombora mawili yaliyofyatuliwa kutoka Iran kuelekea Kuwait yalipoteza mwelekeo au yalivunjika yakiwa angani, huku makombora matatu yaliyolengwa Bahrain yakidunguliwa haraka na mifumo ya ulinzi wa anga ya Marekani na Bahrain."
Iran imekuwa ikifanya mashambulizi mara kwa mara dhidi ya malengo yaliyopo Bahrain na Kuwait, ambako kuna vituo vya kijeshi vya Marekani.
Mapema, CENTCOM ilisema ilikuwa imeishambulia na kuisimamisha meli iliyokuwa ikielekea Iran, ambayo haikuwa imebeba mzigo wowote. Hatua hiyo ilikuwa sehemu ya mzingiro wa kijeshi wa majini wa Marekani katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, ulioanza tarehe 13 Aprili.
Kwa mujibu wa CENTCOM, ndege ya kijeshi ya Marekani ilirusha kombora la aina ya Hellfire katika chumba cha injini cha meli hiyo yenye bendera ya Botswana, baada ya wafanyakazi wake "kupuuza maonyo ya mara kwa mara."
CENTCOM pia ilitoa video ambayo ilisema inaonesha wakati meli hiyo ilipolengwa siku ya Jumanne.
Mvutano unaoongezeka unakuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuwaambia wakosoaji wake wiki hii "watulie na wasiwe na wasiwasi," akisema kwamba Iran "inataka sana makubaliano, na yatakuwa makubaliano mazuri yatakayoinufaisha Marekani."
Vyombo vya habari vya Marekani viliripoti hapo awali kwamba Trump alikuwa ameomba kufanyika kwa mabadiliko katika masharti ya makubaliano ya amani , baada ya kukutana na washauri wake wakuu kujadili upanuzi wa mfumo wa kusitisha mapigano.
Kama ilivyoripotiwa na CBS News, mabadiliko yaliyopendekezwa yalihusu Mlango wa Bahari wa Hormuz, kuondolewa kwa urani ya Iran iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu, pamoja na kuweka utaratibu wa kuanzisha tena mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Jumatatu, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alikanusha kwamba masuala hayo yalikuwa sehemu ya mazungumzo, akiongeza kuwa Washington "hubadilisha msimamo wake kila mara na daima huwasilisha madai mapya au yanayokinzana."
Katika taarifa yake ya hivi karibuni, CENTCOM ilisema kwamba vikosi vya Marekani vilitekeleza hatua za mzingiro dhidi ya meli ya M/T Lexie yenye bendera ya Botswana wakati ilipokuwa ikipitia maji ya kimataifa ikielekea Kisiwa cha Kharg.
Ilisema wafanyakazi wa meli hiyo walishindwa kutii maagizo ya jeshi la Marekani mara kadhaa ndani ya kipindi cha saa 24.
Kwa ujumla, CENTCOM ilisema kuwa meli sita za kibiashara zimezuiwa kufanya shughuli tangu mzingiro huo ulipoanza, huku meli nyingine 122 zikielekezwa kwenye maeneo mengine.
Shirika la habari la BBC lilisema kuwa limewasiliana na serikali ya Botswana ili kupata maoni yake kuhusu suala hilo.
Mapambano ya hivi karibuni yalitokea wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alipofanya kikao chake cha kwanza rasmi mbele ya Bunge la Marekani tangu vita hivyo vianze.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani alieleza katika ushahidi wake kwamba mazungumzo ya Marekani hayakuipa Iran ahueni ya vikwazo vya kiuchumi kwa masharti ya kufungua tena Mlango wa Bahari wa Hormuz.
"Kwa sasa, kila jambo ambalo limejadiliwa nao linategemea msingi kwamba ahueni yoyote ya vikwazo itakuwa na masharti. Hii ina maana kwamba hatua kama hiyo itafanyika tu ikiwa sababu za awali za kuwekwa kwa vikwazo zitashughulikiwa, ambazo ni mpango wao wa nyuklia," alisema.
Katika mahojiano mengine yenye mvutano mkali na mmoja wa maseneta, Rubio alisema:
"Vita vimekwisha."
Wajumbe wa kamati hiyo waliuliza maswali magumu kuhusu mkakati wa Marekani wa kumaliza mzozo huo, wakitaka kujua jinsi serikali inavyopanga kuhakikisha kuwepo kwa amani ya kudumu na utulivu katika eneo hilo.