Tshisekedi amshutumu Kabila kwa kugeuka dhidi ya wananchi aliowaongoza
“Sielewi jinsi mtu aliyewahi kuongoza nchi yenye mamilioni ya wananchi anavyoweza kutawaliwa na hasira, kushindwa kujizuia, kuchukua silaha na kuzitumia dhidi ya watu aliowaongoza kwa miaka 18.”
Hayo ni maneno ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, akimzungumzia mtangulizi wake, Joseph Kabila, ambaye hivi karibuni alitangaza kuongoza muungano mpya wa kisiasa na kijeshi ulioundwa mapema mwezi huu kwa lengo la kupambana na serikali ya Kinshasa, ukichukua nafasi ya AFC/M23.
Akizungumza na wabunge wa chama chake tawala mwishoni mwa wiki iliyopita, Tshisekedi alisema hakushangazwa na uamuzi wa Kabila kuvunja ukimya wake, lakini akadai kuwa Rwanda inamtumia.
Tangu kutangazwa rasmi kwa muungano huo mpya, hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa DRC kutoa kauli hadharani kuhusu kuundwa kwake au kuhusu Joseph Kabila.
Serikali ya Rwanda haijatoa maoni kuhusu matamshi hayo ya Tshisekedi.
BBC ilimtafuta Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, ili kupata maoni yake. Katika ujumbe mfupi wa maandishi, alijibu: “Hatujawahi kuwa tukijibu kila anachosema Tshisekedi kuhusu Rwanda.”
Katika hotuba yake, Tshisekedi aliishutumu Rwanda na Rais wake, Paul Kagame, kwa kuhusika katika vita vinavyoendelea mashariki mwa DRC. Pia alidai kuwa Rwanda inamtumia Kabila katika juhudi zake za kuendeleza mzozo huo.
Kwa mujibu wa Tshisekedi, kuundwa kwa vuguvugu la FRN ni njama ya Rwanda ya kuushawishi jumuiya ya kimataifa iamini kuwa mzozo huo ni suala la ndani la Wakongo, badala ya kutambua nafasi ya Rwanda katika mgogoro huo.
Alisema hatua za kidiplomasia zilizochukuliwa na serikali yake zimeisaidia kuonyesha kuwa Rwanda inaikandamiza DRC, hali ambayo, kwa madai yake, imesababisha nchi hiyo kukabiliwa na vikwazo.
Tshisekedi alisema:
“Ndiyo maana ilimwomba mfanyakazi wake aliyekuwa gerezani atoke nje na kuchukua jukumu la uhalifu huu, kwa sababu ilikuwa muhimu kuleta taswira kwamba hili ni suala la Wakongo wenyewe.”
“Kwa hiyo, ilimbidi atoke mafichoni na kuchukua mambo mikononi mwake, ili kuonyesha kuwa huu ni mzozo kati ya Wakongo wenyewe. Namshukuru Mungu, hakuna asiyejua ukweli huo.”
Alisema kilichomvutia zaidi ni namna wananchi walivyoungana kupinga hatua hizo.
“Kilichonivutia zaidi ni kuona wananchi wetu, wanasiasa na raia wa kawaida, wakiungana kulaani vitendo hivi.”
Tshisekedi anaamini kuwa Kabila amewasaliti wananchi na nchi aliyowahi kuiongoza. Kwa maoni yake, hatua hiyo inaonyesha kuwa katika miaka 18 aliyokuwa madarakani, Kabila hakuwahi kuonyesha mapenzi ya dhati kwa nchi na wananchi wake.
Aliongeza:
“Kwa sababu ikiwa unaipenda nchi yako na wananchi wake, huwezi kufanya mambo kama haya. Nilitoa mfano wa maisha yangu mwenyewe, kwa kuwa nami nimepitia hali kama hizo. Tulipopambana na makundi mbalimbali yenye silaha yaliyokuwepo nchini humu, hatukuwahi kufikiria kuchukua silaha ili kupigania nchi yetu.”
Tarehe 12 Oktoba, kuundwa kwa FRN kulitangazwa rasmi chini ya uongozi wa Joseph Kabila. Muungano huo ulisema unalenga kuunganisha kile unachokiita “vikosi vya upinzani” ili kukomesha utawala unaodai kuwa wa kidikteta na kuweka mwelekeo mpya wa kisiasa nchini humo.
Kabla ya Tshisekedi kutoa kauli yake kuhusu Kabila na FRN, serikali yake haikuwa imetangaza hadharani msimamo wake kuhusu muungano huo. Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wanaoshirikiana na serikali walikuwa wameikosoa hatua ya Kabila kuongoza kundi hilo lililochukua nafasi ya AFC/M23.
Ubelgiji, iliyokuwa mtawala wa kikoloni wa DRC, pia imekosoa kuundwa kwa muungano huo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Maxime Prévot, alisema ni “jambo la kusikitisha sana” kuona kiongozi wa zamani wa nchi aliyewahi kukabiliwa na madhara ya makundi yenye silaha akiamua kuongoza muungano wa kisiasa na kijeshi unaolenga kutwaa madaraka kwa kutumia nguvu.
Soma Zaidi: