WhatsApp yatumika kuhamisha mamilioni ya euro kwa wahalifu na magaidi

    • Author, Andy Verity
    • Nafasi, Mwandishi wa Uchunguzi wa BBC News
    • Author, Joseph Lee
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Mawasiliano ya mtandao wa WhatsApp yalitumika kutuma mamia ya mamilioni ya euro kwa fedha taslimu duniani kote, yakichangia uhalifu uliopangwa na ugaidi bila kumbukumbu ya karatasi, imetolewa na uchunguzi uliofanywa na watangazaji barani Ulaya.

Mawasilinao ya kundi la watu 532, lililoitwa "Traders of Greater Europe", kilitumika kupanga uhamishaji wa fedha taslimu kwenda nchi za wateja wao, ikiwemo miji ya Uingereza kama Birmingham na London.

Katika kisa kimoja, malipo kutoka Brussels yalifikia wanamgambo wa kikundi cha Islamic State (IS) nchini Syria.

Mtandao wa uandishi wa uchunguzi wa umoja wa watangazaji wa Ulaya (EBU), unaojumuisha BBC, pia ulibaini ushahidi mpana wa mifumo sawa ya uhamishaji wa fedha ikitumika kwa usafirishaji haramu wa binadamu na biashara ya dawa za kulevya.

Mawasilano, ya Whatsap yenye zaidi ya ujumbe 82,000 uliotumwa kati ya mwishoni mwa Februari na Desemba 2022, yaligunduliwa kwanza na hakimu wa uchunguzi wa Ubelgiji Vincent Guerra. Hakimu wa uchunguzi ni hakimu anayechambua ushahidi katika kesi ngumu kabla ya kesi kuanza kusikilizwa na kutoa mapendekezo iwapo wanaweza kusona mbele.

Guerra alisema idadi ya manunuzi ilikuwa 'ya kushangaza' na mtandao ulikuwa 'unahusisha sayari nzima' (ya dunia). Kesi ilianza kama uchunguzi wa ufadhili wa ugaidi, lakini 'ikawa ni tone tu katika bahari ya manunuzi', alisema.

Wanakundi wa mawasiliano hayo walituma ujumbe kwa lugha ya Kiarabu kati yao kupanga malipo ya fedha taslimu kwa kutumia mfumo wa zamani wa uhamishaji wa hawala. Hawala inahusisha mtandao wa madalali wa fedha waliothibitishwa ambao wanaweza kupanga fedha kutumwa kote duniani bila kikomo kwa njia ya elekroniki au usafirishaji wa fedha taslimu.

Mfumo huu unahusisha makubaliano kati ya madalali wawili, yanayojulikana kama hawaladars, katika maeneo tofauti. Mojawapo ya hawaladars anapokea kiasi cha fedha taslimu na mwingine anakubali kutoa kiasi sawa, pungufu ya kamisheni, kwa mpokeaji. Hawaladars wanakubali kulipana manunuzi yote kati yao baadaye.

Uhamishaji wa hawala mara nyingi hutumika kwa madhumuni halali, kama vile wafanyakazi wahamiaji kutuma fedha nyumbani kusaidia familia zao katika nchi zenye matumizi hafifu ya benki

Lakini wahalifu pia wanaweza kutumia uhamisho wa hawala kuepuka mfumo wa Swift unaotumika kuhamisha fedha za kimataifa, ambapo benki kwa kawaida hubainisha miamala mikubwa isiyo ya kawaida kuhusu biashara na zinatakiwa kuripoti shughuli zozote zinazohisiwa kama zenye shaka.

Kundi laa wafanyabiashara wa Ulaya lilikuwa mahususi ya kwa miamala ya zaidi ya €5,000 (£4,279) na malipo mara nyingi yalikuwa makubwa zaidi ya hapo. Hakuna dalili kwamba wote waliokuwa sehemu ya kikundi walihusika katika kushughulikia fedha haramu.

Hawala ni haramu katika nchi nyingi, ikiwemo sehemu kubwa za EU, lakini ni halali Uingereza mradi tu wakala wakiwa wamejisajili na Mamlaka ya Mapato na Mizani (HMRC).

Ujumbe wa WhatsApp uligunduliwa na EBU kufuatia kesi ya mwaka 2024 nchini Ubelgiji ambapo washtakiwa sita wa utakatishaji wa fedha walihukumiwa, wakiwemo Abu Adam, kiongozi wa mtandao huko Brussels, na mshirika wake, Abu Ahmed.

Polisi wa Ubelgiji waligundua ushahidi kwamba washtakiwa walikuwa wakituma fedha kwa IS, ambazo zilitumwa kusaidia wake wa wanamgambo kukimbia kutoka kwenye kambi za vifungo nchini Syria. Walipomkamata Abu Adam, waligundua mawasiliano ya kikundi cha Traders of Greater Europe kwenye simu yake.

Guerra alisema ilikuwa kama "kupata bahati kubwa", kugundua jinsi mfumo mkubwa na wa siri nyingi unavyofanya kazi. Simu hiyo pia ilikuwa na picha 6,000 za noti za €5 zikionesha nambari za mfuatano na picha 6,000 za kadi za utambulisho. Maelezo haya mara nyingi hutumika kama nambari za kipekee za utambulisho katika miamala ya hawala, na jumla ya noti na kadi za kitambulisho zinaonesha Abu Adam alikuwa amefanya walau miamala 12,000, alisema Guerra.

"Hii si kazi ya ridhaa; ni ya kitaalamu, na kwa kiwango ambacho hatungeweza kudhani," alisema. "Wao ni benki bila usimamizi wa serikali."

EBU pia iligundua makundi zaidi barani Ulaya yanayotumia mfumo wa hawala kwa shughuli za uhalifu. Mmoja wa wahusika wa zamani wa utakatishaji fedha aliyewahi kuwa katika mitandao ya hawala ya Ulaya, anayeitwa Frank, aliimbia EBU kwamba alikuwa amehusika katika miamala yenye jumla ya mamia ya mamilioni ya euro.

Utambulisho wake wa kwanza kwa mfumo wa hawala ulikuwa katika ofisi katika mji mdogo kando kidogo ya Rotterdam, alisema. Hapo, watoaji wanne au watano walifika na fedha ndani ya takriban saa moja na nusu, wakihamisha fedha zisizopungua euro milioni moja, alisema.

"Niligundua baadaye ni kwamba si tu kuhusu fedha. Ni kuhusu ufadhili wa ugaidi. Ni kuhusu biashara ya dawa za kulevya. Ni kuhusu utumwa wa ngono na mambo mengine yote ya ovyo, tuseme kwa njia nzuri," alisema.

Mifumo ya kesi nchini Austria pia imeonesha jinsi mfumo wa hawala unavyohusishwa na biashara haramu ya binadamu watu na vurugu.

Katika kesi moja iliyochunguzwa na kituo cha utangazaji nchini Austria (ORF), sehemu ya mtandao wa EBU, polisi wa Austria walifanya msako katika kile walichokiita "ofisi kubwa zaidi ya hawala Vienna". Iliyoendeshwa kwenye mgahawa wa kebab kwenye barabara yenye shughuli nyingi na ambao mamlaka walisema ulitumiwa kufanya malipo biashara ya binadamu.

Ndugu wawili wa Syria waliokuwa wakihusika operesheni hiyo walishtakiwa kwa biashara ya binadamu, pamoja na kutesa na kumbaka mhamiaji ambaye alikuwa amepoteza €350,000 (£300,000), wakisema aliibiwa. Walihukumiwa mwaka jana na kupewa kifungo cha miaka 18 na 8 jela mtawalia.

Polisi wa Austria na Europol pia hivi karibuni walisambaratisha mtandao wa bishara ya binadamu kupitia hawala, ambacho maafisa walisema kilisafirisha watu takriban 100,000 kwenda Ulaya kwa kipindi cha zaidi ya miezi 18.

Gerald Tatzgern, anayeongoza uchunguzi wa biashara ya binadamu katika Taasisi ya Ujasusi wa Jinai ya Austria, BK, aliiambia ORF kwamba utesaji ni halisi katika biashara ya binadamu na pia hutumika kuongeza faida.

Alisema: "Video za utesaji baadaye hutumwa kwa familia, zikisema kwamba iwapo hawatatuma euro 1,000 zaidi au maelfu kadhaa ya euro, basi mhusika - mtoto wako, kaka yako, baba yako - atakumbana na mateso."

Gerald Tatzgern alisema magenge yaliwatesa wahamiaji na kuomba fedha kutoka kwa familia zao kupitia mfumo wa hawala.

Malipo ya kuacha ukatili yalikuwa yakihitajika kupitia mfumo wa hawala, alisema.

Kamanda wa polisi pia afisa wa kiungo na Polisi wa Ulaya (Europol), Quentin Mugg, ambaye amesimamia uchunguzi kadhaa wa utakatishaji fedha, alisema mfumo wa hawala ulikuwa "njia kuu ya kutakatisha fedha kwa uhalifu uliopangwa."

"Haijalishi fedha zinatoka kwenye usafrishajin wa wahamiaji, biashara ya binadamu, akiba ya bibi inayotumwa kama zawadi ya siku ya kuzaliwa kwa mtoto wake, au mali ya anayeishi Ufaransa anayetaka kuisaidia familia yake, (mahawala) hawajali kabisa," alisema. "Na watatumia viwango vyao."

Imetafsiriwa na Florian Kaijage